Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeripoti idadi ya watu walioambukizwa na maradhi ya homa ya mafua ya nguruwe imeongezeka, kwa kulingana na taarifa ilizopokea Ijumatano kutoka maabara ya uchunguzi wa kisayansi wa maradhi.

Jumla ya wagonjwa waliothibitishwa rasmi kisayansi kuambukizwa na virusi vya homa ya nguruwe ya aina ya A/H1N1 Ijumanne ilikuwa ni wagonjwa 79, wakati jumla ya wagonjwa siku moja baadaye imesajiliwa kufikia 114. Shirika la WHO linahadharisha virusi vya homa ya mafua ya nguruwe vinatapakaa na kuenea kwa kasi katika nchi mbalimbali, nje ya Amerika ya Kaskazini, maeneo ambayo inakadiriwa kulipochipuka maradhi haya, na hakuna dalili sasa hivi zenye kuonyesha kasi ya maambukizi ya virusi hivyo inateremka. Dktr Margaret Chang, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwenye mkutano aliokuwa nawo na waandishi habari wa kimataifa Ijumatano (29/04/2009) usiku, mjini Geneva, alitangaza rasmi kwamba daraja ya hadhari ya maambukizi ya homa ya mafua ya nguruwe imelazimika kupandishwa tena kutoka daraja ya nne na kuwa daraja ya tano, kwa sababu ya kukithiri kwa kasi ya maambukizi, kasi ilioyakinika kujiri kimataifa sasa hivi. Wakati huo huo Dktr alizihimiza "nchi zote wanachama kufufua, kidharura, miradi yao ya kitaifa ya kukabiliana na mripuko wa janga la maradhi linalosambaa kwa kasi katika sehemu mbalimbali za dunia" na pia kuzisihi nchi zote kuendeleza uangalizi wa kiwango cha juu kabisa, ili kusaidia huduma za kudhibiti bora afya ya jamii dhidi ya hatari ya kuenea kwa virusi vya H1N1 kwenye maeneo yao." Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza kwamba limelazimika kupandisha kiwango cha hadhari ya maambukizo kutoka daraja ya nne hadi daraja ya tano, ikimaanisha maambukizi ya maradhi yamedhihirika, kwa ushahidi usiokatalika, kutukia kati ya wanadamu, na kusarifika katika nchi mbili ziliomo kwenye ukanda unaofuatiliwa kitaalamu na WHO.

Baraza la Usalama lilikutana leo Makao Makuu, kwenye kikao maalumu cha hadhara kilichoitishwa na Mexico, kuzingatia taratibu za kukomesha vitendo karaha na kusitisha madhara ya mateso dhidi ya watoto walionaswa kwenye mazingira ya mapigano na uhasama. Mkutano ulioongozwa na Waziri wa Nchi za Kigeni wa Mexico, Patricia Espinosa ambaye taifa lake ndio limeshika uraisi wa Baraza kwa mwezi Aprili. Kwenye risala alioiwakilisha mkutanoni KM Ban Ki-moon alihimiza mataifa, kwa ujumla, kuandaa hatua za haraka, kukomesha haraka tabia ya kuajiri kimabavu watoto wadogo na kuwashirikisha kwenye mapigano haramu. Mjumbe wa KM juu ya Hifadhi ya Watoto Walionaswa kwenye Mazingira ya Mapigano, Radhika Coomaraswamy alisihi wajumbe wa Baraza la Usalama wakati umewadia kwa wao kubuni kanuni mpya, zitakazoruhusu kuchapisha majina ya watu wanaofanya vitendo vya kunajisi watoto na udhalilishaji wa kijinsiya na pia kuhakikisha watuhumiwa wa jinai hiyo wanaadhibiwa kisheria. Grace Akallo, aliyelazimishwa kushiriki kwenye mapigano angali na umri mdogo na kundi la waasi wa Uganda la LRA, naye pia alihutubia Baraza la Usalama. Alieleza kwenye hotuba yake namna alivyotoroshwa kimabavu na waasi kutoka bweni la skuli aliokuwa akihudhuria, na baadaye kunajisiwa mara kadha wa kadha na viongozi wa waasi wa LRA wakati alipokuwa kizuizini. Alikumbusha kwamba alipata motisha wa kuhutubia Baraza juu ya maafa yaliomsibu wakati yupo kizuizini, kwa matumaini itasaidia kubainisha "usumbufu halisi na mateso wanayopata idadi kubwa ya wale watoto waliotekwa nyara na makundi yenye silaha, wanaolazimishwa kupigana, watoto ambao wanateswa kila siku." Alisema watoto waathirika wanatarajia kuvuliwa na janga la kuwekwa kizuizini, kudhalilishwa na kulazimishwa kupigana, kinyume na mikataba ya kimataifa na haki ya mtoto, na kuihimiza jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura zitakazowapatia stara na hifadhi wanayostahiki.

Shirika la Vikosi Mseto vya Ulinzi Amani vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) limeanzisha mradi maalumu wa ushirikiano kati ya kitengo chake cha polisi na Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Wanawake (UNIFEM). Elizabeth Muwanga, Naibu Kamishna Polisi wa UNAMID alisema ushirikiano huu mpya utaimarisha mafanikio yaliopatikana katika kurudisha utulivu wa eneo, na utasaidia kuratibu huduma za pamoja ili kusawazisha usalama na amani, kuzalisha ajira na imarisha pia ulinzi wa wahamiaji wa ndani (IDPs) hususan wanawake dhidi ya uonevu, unyanyasaji na matesoya kijinisiya.