Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taarifa mpya za WHO juu ya homa ya mafua ya nguruwe

Taarifa mpya za WHO juu ya homa ya mafua ya nguruwe

Umoja wa Mataifa unaendelea kushughulikia tatizo la afya lililozuka ulimwenguni hivi karibuni, baada ya kugunduliwa homa ya mafua ya nguruwe katika baadhi ya mataifa na namna ugonjwa huu ulivyoathiri wanadamu.

Gregory Hartl, Msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) leo asubuhi aliwaambia waandishi habari wa kimataifa, waliokusanyika kwenye Ofisi ya UM mjini Geneva, ya kwamba WHO imepokea ripoti za kutoka maabara ya uchunguzi wa maradhi, zilizothibitisha kwamba jumla halisi ya watu walioambukizwa kihakika, wakati huo, na homa ya mafua ya nguruwe ilikuwa ni 73, na miongoni mwa idadi hiyo wagonjwa 40 walikutikana Marekani, 26 katika Mexico na wagonjwa wengine 6 walikumbwa na maradhi katika Kanada na mtu 1 aliuguwa nayo Uspeni. Taarifa ya WHO inasema wagonjwa 7 walioambukizwa na homa ya mafua ya nguruwe katika Mexico walishafariki. Taasisi ya afya ya kimataifa ilihadharisha pia kwamba kitendo cha kuchekecha wasafiri kwenye viwanja vya ndege ni kadhia isio na uwezo wa kutupatia matokeo sahihi ya maambukizo. Lakini WHO imeunga mkono ile rai ya Nchi Wanachama, kutekeleza hatua za kizalendo katika kudhibiti afya ya jamii dhidi ya homa ya mafua ya nguruwe, kwa kuwahadharisha raia juu ya namna ya kujikinga na mambukizo ya virusi vya homa. Vile vile WHO imezinasihi serikali zote duniani kuongeza juhudi za uangalizi wa maambukizi ya maradhi katika maeneo yao, kwa kuhakikisha raia wote hupatiwa taarifa zenye maelezo ya hatua za kuchukuliwa nao pindi wamejikuta wameambukizwa na ugonjwa huo. Kadhalika, Serikali wanachama zimehimizwa kuhakikisha kuna akiba ya kutosha nchini ya dawa kinga dhidi ya homa ya mafua ya nguruwe. Hivi sasa maabara manne ya kimataifa yameshiriki kwenye huduma za kutengeneza chanjo kinga dhidi ya maradhi, na kwa mujibu wa ripoti ya WHO dawa hizi hazitokuwa tayari kugawiwa au kutumiwa na wagonjwa mpaka baada ya miezi sita. WHO ilieleza kwamba haina uwezo wa kuyaharakisha maabara haya manne yanayotengeneza chanjo kinga mpaka pale itakapoamuliwa na wataalamu ya kuwa hatari ya mripuko wa maradhi imefikia daraja ya tano ya maambukizo. Hivi sasa hatari ya maambukizo kimataifa ipo kwenye daraja ya nne ya tahadhari. Mataifa Wanachama 150 yameripotiwa kuanzisha miradi ya kizalendo dhidi ya mripuko wa homa ya mafua ya malaria. Miradi hii iliandaliwa kufuatia uzoefu uliopatikana kati ya miaka ya 2003 hadi 2004, pale ulimwengu ulipokabiliwa na mripuko wa ile homa ya mafua ya ndege, iliojulikana kama homa ya SARS.