Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO inahadharisha homa ya nguruwe inahatarisha kuenea kimataifa kama haijadhibitiwa mapema

WHO inahadharisha homa ya nguruwe inahatarisha kuenea kimataifa kama haijadhibitiwa mapema

Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Afya Duniani (WHO) kwenye mahojiano na waandishi wa habari mwisho wa wiki [25/04/2009], alihadharisha mripuko wa karibuni wa aina ya virusi vya homa ya mafua - inayotambuliwa kwa umaarufu kama homa ya mafua ya nguruwe - katika maeneo ya Mexico na Marekani, inatakikana kudhibitiwa mapema, au si hivyo homa hii inaashiriwa itaenea kwa kasi na kudhuru fungu kubwa la umma wa kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, maambukizo mapya ya homa ya mafua ya nguruwe yanadhaniwa ndio yaliosababisha vifo vya makumi kadha ya watu katika miji mitatu iliopo Mexico, na vile vile kusababisha watu wanane kupatwa na ugonjwa huo kwenye majimbo ya Marekani ya California na Texas, yanayopakana na Mexico. Kadhalika, wahudumia afya wanashuku virusi vya homa ya mafua ya nguruwe ilienea pia kwenye majimbo ya New York na Kansas. Kwenye risala mbele ya waandishi habari, Dktr Margaret Chan alionya hali hii hatari imegundulikana kubadilika haraka, na alihadharisha kuwa kunahitajika taarifa kamili juu ya namna maradhi yanavyodhibitiwa kwenye maeneo husika, zitakazoiwezesha jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za dharura kuyadhibiti maradhi yasije yakaenea nje ya maeneo yalioambukizwa nayo kwa sasa hivi. WHO imeripoti kuwa hawezi kubashiria kama mripuko wa sasa, wa homa ya mafua ya nguruwe, huenda ukageuka janga la kudhuru afya ya kimataifa. Lakini alisisitiza kwamba WHO ilifanikiwa kuthibitisha virusi vya maradhi yaliowapata wagonjwa wa Mexico na Marekani kuwa vina nasaba ya vile virusi vya wanyama vya aina ya H5N1, virusi ambavyo pia vimeanza kuambukiza wanadamu, halkadhalika, hali ambayo ina uwezo wa kulieneza janga hili kimataifa, kwa kasi, kama halijadhibitiwa mapema. Wataalamu wa WHO wanaohusika na maradhi ya kuambukiza wameripoti ya kuwa, hadi sasa, wameshindwa kugundua dalili zozoye zenye kuthibitisha kuwa homa ya mafua ya nguruwe imefumka mbali ya zile sehemu ziliotangazwa kuwa nayo sasa hivi. Hata hivyo, Mkurugenzi wa Shirika la WHO, Dktr Margaret Chan amehadharisha walimwengu kwamba "hali iliojiri kiafya, juu ya homa ya mafua ya nguruwe, ni ya hatari sana na inahitajia kuangaliwa, na kudhibitiwa kwa ukaribu sana" na jumuiya yote ya kimataifa, ili kuhakikisha haitozusha janga ovu, na maututi, la afya duniani. Kamati ya dharura, ya utendaji, ya WHO inalizingatia suala la homa ya mafua ya nguruwe sasa hivi na inatazamiwa kutoa uamuzi wake haraka katika wiki hii.