Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Taarifa mpya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), juu ya mripuko wa homa ya mafua ya nguruwe, imesema wataalamu wa taasisi ya afya wamethibitisha virusi vilivyosababisha homa ya mafua ya nguruwe, iliogundulikana karibuni katika mataifa ya Marekani, Mexico na Kanada, ni virusi vya aina ya A/H1N1.

Taarifa hii ilitolewa baada ya kikao cha pili cha Kamati ya Dharura ya WHO kumalizika Ijumatatu, tarehe 27 Aprili 2009 mjini Geneva. Kamati ya Dharura ilibuniwa kwa kuambatana na Kanuni za Afya ya Kimataifa za 2005 kwa madhumuni ya kushauriana juu ya hatua za kuchukuliwa juu ya afya ya jamii pakizuka ghafla maradhi ya kuambukiza yanayohatarisha jamii ya kimataifa. Kufuatia kikao cha Kamati, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Daktari Margaret Chang alitoa uamuzi ufuatao: aliamua kuweka kipimo cha hadhari ya mfumko wa janga la homa ya mafua kwenye kiwango cha juu, kutoka daraja ya 3 na kuwa daraja ya 4 ya hadhari. Mageuzi haya yanamaanisha kukithiri kwa uwezekano wa janga la homa ya mafua ya nguruwe kufumka ulimwenguni, na haimaanishi tukio hili haliepukiki. Uamuzi wa Kamati ya Dharura ya kupandisha daraja ya hatari ya maambukizo ya maradhi unatokana na vipimo vya afya, vilivyothibitisha maradhi haya huambukizwa kutoka mwanadamu mmoja hadi mwengine, na sio kutoka wanyama, hali ambayo inahatarisha janga la maradhi kuripuka kwa kasi yenye uwezo wa kudhuru fungu kubwa la jamii ya wanadamu. Ilivyokuwa maradhi yameonekana kutapakaa katika maeneo tofauti duniani, kwa kiwango kidogo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO ameamua mripuko wa homa ya mafua ya nguruwe hautofanikiwa kuzuilika kikamilifu, na kwa hivyo alipendekeza juhudi za kuhudumia udhibiti wa jumla zilengwe zaidi kwenye zile hatua za kupunguza kasi ya maambukizi ya maradhi kila yanapoibuka kwenye maeneo husika. Wakati huo huo aliyasihi mataifa kutofunga mipaka, wala kupiga marufuku watu wasisafiri nje.

Kwenye Mkutano wa Wawakilishi wa Hadhi ya Juu ulioandaliwa na Baraza la Uchumi na Jamii pamoja na Taasisi za Bretton Woods (kama Benki Kuu ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa n.k) na pia mashirika mengine yanayohusika na maendeleo ya uchumi wa kimataifa, KM alieleza juu ya umuhimu wa kikao cha mwaka huu katika juhudi za kuchangisha suluhu ya kuridhisha, inayotakikana kutatua mizozo ya kiuchumi na jamii ilioufunika ulimwengu sasa hivi. Alikumbusha mgogoro wa uchumi na jamii, uliojiri duniani leo hii, umebainisha kidhahiri kabisa udhaifu hatari uliopo na dosari kuu ya mfumo wa uchumi wa kimataifa.

Rodolpho Adada, Mkuu wa Shirika wa UM juu ya Operesheni za Kulinda Amani Darfur za Vikosi vya Mchanganyiko vya UM na UA, yaani vikosi vya UNAMID, alipohutubia Baraza la Usalama Ijumatatu asubuhi alieleza mzozo wa jimbo la magharibi la Sudan sasa hivi unawakilisha "mvutano wa wote dhidi ya kila mtu" na wakati huo huo vikosi vya Serikali vimeamua "kupambana na makundi ya waasi wenye silaha, ambao nao vile vile wanapigana wao kwa wao, ikichanganyika na mapigano ziada ya kikabila."

UNAMID imetangaza Naibu Kamanda Mkuu wa vikosi vya UNAMID, Meja-Jenerali Emmanuel Karake Kenzi, raia wa Rwanda, aliyelitumikia shirika tangu Januari 2008, anatarajiwa kumaliza muda wake Darfur katika siku za karibuni. Nafasi yake imeripotiwa itachukuliwa na Meja-Jenerali Duna Dumisani wa Afrika Kusini