Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

John Holmes, Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu na Mratibu wa Misaada ya Dharura anatazamiwa mwisho wa wiki kufanya ziara ya siku tatu katika Sri Lanka. Anatazamiwa kuwa na mazungumzo muhimu na maofisa wa Serikali ya Sri Lanka, ikijumlisha masuala yanayohusu uwezekano wa kuipatia UM kibali cha kupeleka watumishi wae kufanya makadirio ya hali na mahitaji ya umma kwenye eneo la uhasama. Holmes pia atazungumza na wenye mamlaka juu ya namna ya kuwafikia raia waliopo kwenye vituo vya ukaguzi vya Serikali ili kuwahudumia kihalio, na wakati huo huo kuisihi Serikali kuwaachia huru watumishi wa UM waliopo vizuizini. Halkadhalika, Mratibu Mkaazi wa UM juu ya Misaada ya Kiutu katika Sri Lanka, Neil Buhne leo alitazamiwa kuelekea mji wa Jaffna, uliopo Sri Lanka kaskazini, akiongoza ujumbe wa UM uliodhaminiwa madaraka ya kuchunguza hali halisi ilivyo kwenye eneo la vurugu.

KM Ban Ki-moon ameripotiwa kulaani vikali mashambulio ya mabomu ya kujitoa mhanga yaliofanyika Alkhamisi na Ijumaa kwenye miji ya Baghdad na Dyala, Iraq na kuua watu wanaokadiriwa 150, ikijumlisha idadi kubwa ya raia wa kutoka Iran, waliokuwa wakifanya ziara za ibada nchini Iraq. KM alizitumia aila za waathirika wa tukio hilo mkono wa taazia, na alisema pia kuchukizwa sana na ripoti zenye kudai kwamba mmoja wa washambuliaji wa mabomu ya mhanga alikuwa mwanmke aliyebeba mtoto wa miaka mitano! KM alishtumu na kusisitiza ya kuwa kwa kulingana na mawazo yake pamoja na maadili ya kiutu, anaamini hakuna sababu yoyote ile wala malalamiko yanayostahili kitendo kama hicho dhidi ya umma usio hatia.

Baraza la Usalama lilikutana asubuhi Makao Makuu kwenye mkutano wa hadhara kuzingatia hali ya amani katika mataifa ya Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Shirika la Kimataifa juu ya Mawasiliano ya Simu (ITU) limemaliza majadiliano kwenye ule warsha maalumu uliofanyika kwenye mji wa Lisbon, Ureno kuzingatia sra za mawasiliano mapya ya simu duniani. Miongoni mwa maafikiano yaliojumuishwa mkutanoni ni ile rai iliotangazwa rasmi na Hamadoun Touré, Mkuu wa Shirika la ITU, kuanzisha skuli za mtandao za kimataifa, zitakazowafadhalia watoto wa nchi zinazoendelea kompyuta ndogo ndogo kwa masomo. Kadhalika ilitiliwa mkazo kwamba wakati umewadia kwa umma wa kimataifa kueneza "Mradi wa Marshall ya mawasiliano ya kisasa" utakaokuwa na natija kwa umma katika kila pende ya dunia. Touré alisema walimwenguwamehsatambua kihakika, katika kipindi cha hivi sasa, ya kuwa uwezo wa kufikia,kwa urahisi, habari na taarifa za kina zinazofungamana na teknolojia ya mawasiliano ya kisasa ndio kadhia muhimu zenye uwezo wa kuzalisha ajira na kuongoza ukuaji wa haraka wa maendeleo ya kiuchumi na jamii kwa ujumla, hususan katika nchi masikini.