Hapa na pale

Hapa na pale

Kundi la FNL la waasi wa Burundi limetambuliwa rasmi na Serikali, mnamo tarehe 21 Aprili 2009, kuwa kama ni chama halali cha siasa baada ya kufanikiwa kujitenga na mapigano; na baada ya kuridhia kuwakabidhi wenye mamlaka silaha na pia kuachia huru wale watoto waliolazimishwa kushiriki kwenye mapigano. KM Ban Ki-moon alipongeza uamuzi wa kundi la FNL la kuacha mapigano. Mwelekeo mpya huu wa wafuasi wa FNL umewapatia fursa ya kujishirikisha, kikamilifu, kwenye mfumo wa kidemokrasia nchini.

Ripoti ya KM juu ya Usomali, iliotolewa rasmi wiki hii, ilijumlisha matokeo ya uchunguzi uliofanywa na jamii ya kimataifa katika kutafuta taratibu zinazofaa kufuatwa na UM, ili kuyatekeleza mapendekezo ya azimio 1863 (2009) ya Baraza la Usalama ya kuanzisha operesheni mpya za kulinda amani Usomali kwa mafanikio. Kwa mujibu wa ripoti hatua hii haitotimizwa mpaka baada ya Baraza la Usalama kutoa uamuzi juu ya suala hilo mnamo tarehe 1 Juni 2009. Ripoti ya KM inasema operesheni za kulinda amani Usomali sizianzishwe nchini kabla ya, kwanza, kukamilisha majukumu yanayohitajia kupitia awamu tatu za utendaji - majukumu ambayo yanahusu ujenzi wa taasisi za kizalendo za ulinzi na usalama, uimarishaji wa mfumo wa kisiasa nchini na, hatimaye, kuhakikisha Timu ya Watumishi Wakazi wa UM katika Usomali watakuwa na uwezo wa kuendeleza shughuli za kuhudumia misaada ya kiutu nchini bila matatizo.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeripoti Serikali ya Sudan Kusini sasa imeanzisha hatua za dharura zenye dhamira ya kuzuia mripuko wa maradhi ya kupooza (polio) kuenea kwenye Pembe ya Afrika. Kabla ya hapo polio ilikutikana kwenye sehemu za Sudan Kusini na Ethiopia magharibi. Lakini mwaka huu maradhi haya vile vile yamegunduliwa katika sehemu za Sudan kaskazini, Kenya na Uganda.

Robert Serry, Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani kwa Mashariki ya Kati Ijumanne alizuru sehemu za Jerusalem Mashariki na kushuhudia nyumba za WaFalastina zilizobomolewa na ambapo pia nyumba nyengine za WaFalastina zimeonekana kutayarishwa kuvunjwa na wenye mamlaka Israel. Serry alisikitishwa na uvunjaji nyumba za WaFalastina uliofanyika siku ya leo. Aliisihi Serikali ya Israel kusimamisha vitendo hivi na kujitahidi kutimiza zile ahadi ilizotoa siku za nyuma, kwa kulingana na mapendekezo ya Ramani ya Mapatano ya Amani. Serry alisisitiza vitendo vya Israel kuvunja nyumba za WaFalastina huathiri sana kimaisha WaFalastina wa kawaida, na hupalilia hali ya wasiwasi katika mji wa Jerusalem, na kwa wakati huo huo pia kudhoofisha juhudi za kujenga hali ya kuaminiana.