Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fujo za kikabila Sudan Kusini zaitia wasiwasi UNMIS

Fujo za kikabila Sudan Kusini zaitia wasiwasi UNMIS

Shirika la UM Linalosimamia Ulinzi wa Amani Sudan Kusini (UNMIS) limeripoti kuingiwa wasiwasi mkuu kuhusu usalama wa eneo, baada ya kufufuka tena kwa mapigano ya kikabila kwenye Jimbo la Jonglei, ambapo inaripotiwa mnamo mwisho wa wiki iliopita darzeni za watu waliuawa, wenziwao kadha wa kadha walijeruhiwa na wengine kulazimika kukimbia makazi na kuelekea kwenye maeneo jirani.

Kwenye taarifa kwa waandishi habari UNMIS imesihi "makundi yote yanayohasimiana kujizuia, haraka iwezekanavyo, na matumizi ya mabavu" na pia kuwataka viongozi wa jamii na makabila ya kusini kujitahidi "kusuluhisha tofauti zao kwa mazungumzo ili kuleta amani, kama ilivyopendekezwa na Maafikiano ya Jumla ya Amani" yaliotiwa sahihi na Serikali ya Muungano wa Taifa na Serikali ya Sudan Kusini, mwafaka uliosaidia juhudi za kusimamisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, baina ya kaskazini na kusini, yaliopamba nchini humo kwa muda wa zaidi ya miaka ishirini.