Mjumbe wa KM anabashiria askari watoto wataachiwa na waasi katika JKK
Radhika Coomaraswamy, Mjumbe Maalumu wa KM Anayehusika na Hifadhi ya Watoto kwenye Mazingira ya Mapigano ameripoti kuwepo maendeleo ya kisiasa ya kutia moyo hivi karibuni, katika JKK, ambayo alisema yamewakilisha fursa mpya itakayosaidia kuharakisha kuachiwa huru wale askari watoto waliokuwa wakidhibitiwa na makundi ya waasi wanaochukua silaha.
Mapema wiki hii, kwenye mahojiano na waandishi habari, baada ya kumaliza ziara yake katika JKK, Coomaraswamy alinakiliwa akisema ya kuwa tangu mwezi Januari mwaka huu, askari watoto 1,200 walifanikiwa kuachiwa huru na majeshi ya mgambo, vikosi ambavyo sasa vinajiunga rasmi na Jeshi la Taifa la Kongo katika eneo la Kivu Kaskazini, kufuatia maafikiano ya kurudisha utulivu wa eneo.