Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

Mataifa Wanachama yanayohudhuria Mkutano wa Mapitio ya Mwito wa Durban Kupinga Ubaguzi Duniani, unaofanyika wiki hii Geneva, Ijumanne yalipitisha, kwa ridhaa ya wote, ule waraka wa mkutano, hatua ambayo ilipongezwa kidhati na KM Ban Ki-moon.

Kwenye mahojiano aliokuwa nayo baadaye na waandishi habari, KM alisema maafikiano ya kupitisha waraka wa mkutano ni kitendo kitakachohamasisha jumuiya za kimataifa kutekeleza ahadi walizotoa kuambatana na Mpango wa Utendaji wa Azimio la Durban (DDPA), na kuwapa matumaini mamilioni ya waathiriwa wa ubaguzi wa rangi, ukabila, chuki ya wageni na utovu wa kuvumiliana kitamaduni unaohusikana na vitendo kama hivyo vilivyojiri kote duniani. Alisisitiza KM kwamba mradi wa kupiga vita ubaguzi wa rangi ni utaratibu wa muda mrefu. Alitumai Mataifa Wanachama yaliosusia kikao cha Geneva yatajiunga tena haraka na jumuiya ya kimataifa, kwenye zile juhudi za kupambana na janga la ubaguzi wa rangi na ukabila.

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu vile vile aliongeza sauti yake kwa kupongeza maafikiano ya waraka wa Mkutano wa Mapitio dhidi ya Ubaguzi, kitendo alichokitafisiri kama ni tukio kuu la kihistoria, liliofanikiwa kukamilisha mashauriano yaliochukua muda mrefu yenye natija kwa umma wa kimataifa. Mfumo wa waraka wa mkutano, alikumbusha Pillay, huchangisha vipengele muhimu mbalimbali. Mathalan, maafikiano ya waraka yamejumuisha mwongozo wa kuzihamasisha nchi wanachama kutekeleza kihakika zile ahadi walizotoa siku za nyuma juu ya Mpango wa Utendaji wa Azimio la Durban (DDPA); waraka pia umethibitisha taarifa zinazoelezea kuongezeka kwa vitendo vya mateso dhidi ya jamii mbalimbali zilizosumbuliwa na ubaguzi kufuatia kikao cha Durban cha 2001 cha kupinga ubaguzi. Kwa mujibu wa Pillay waraka umeweza kufafanua taratibu zinazofaa kuchukuliwa kitaifa na kimataifa ili kupambana vizuri zaidi na matatizo ya ubaguzi. Waraka vile vile unasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sheria zinazohifadhi uhuru wa kusema na kujieleza; na wakati huo huo waraka umelaani tabia ya kusaliti watu kwa sababu ya itikiadi na imani tofauti za kidini; na waraka wa mkutano pia umejumlisha taratibu za kutumiwa kutathminia namna uchochezi wa chuki (za kikabila, kidini, kimawazo n.k.) unavyotumiwa kugawanya jamii katika sehemu mbalimbali za dunia. Hali kadhalika, Pillay alisisitiza waraka wa mkutano haujaingiza taarifa za aina yoyote zinazozingatia masuala yanayohusu kashfa au uharibifuu wa jina la dini, kinyume na madai ya baadhi ya vyombo vya habari kwamba mada hizo zimejumuishwa ndani ya waraka!

Ripoti ya karibuni ya KM juu ya operesheni za amani katika Darfur, zinazoendelezwa na vikosi vya mchanganyiko vya UM-UA (UNAMID) inabashiria maendeleo yasiotia moyo kwenye huduma za kukidhi mahitaji ya kihali ya umma, baada ya Serikali ya Sudan kupiga marufuku nchini mashirika 16 yanayohusika na haki za binadamu na ugawaji wa misaada ya kiutu kwa jimbo la magharibi la Darfur. Ripoti inasema uamuzi wa Sudan unahatarisha maisha ya umma muhitaji unaokadiriwa watu milioni moja. KM ameiomba Serikali ya Sudan kuzingatia tena rai ya kuwaruhusu wahudumia misaada ya kiutu wa mashirika yasio ya kiserikali, kurejea nchini kuendeleana shughuli zao, hasa ilivyokuwa kuanzia majira ya mvua yanatabiriwa kujongelea na yataanza mwezi ujao, na mchango wa mashirika ya kiserikali ni muhimu katika kuukinga umma na matatizo ya kihali. Inakhofiwa hali huenda ikaharibika zaidi pindi wahudumia misaada ya kiutu wa mashirika yasio ya kiserikali hawatoruhusiwa kurejea haraka kwenye eneo. Ripoti ya KM juu ya operesheni za UNAMID itazingatiwa rasmi Ijumatatu ijayo na wajumbe wa Baraza la Usalama.

Kwenye ripoti nyengine ya KM kuhusu operesheni za Shirika la UM la Kudhibiti Amani kati ya Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINURCAT) imebainisha ya kuwa kwa hivi sasa ni wanajeshi 2000 tu walioweza kupelekwa kwenye eneo hilo, kati ya jumla ya wanajeshi 5,200, idadi iliopendekezwa na Baraza la Usalama. Wakati huo huo ripoti ilisema UM bado unapata matatizo katika kufadhiliwa msaada wa vifaa na silaha zinazohitajiwa na vikosi vya MINURCAT kuendesha kazi zao, mathalan, ndege za helikopta na vifaa vyengine vya kijeshi. Ripoti ya KM imedhihirisha kwamba kati ya ndege za helikopta 18 zinazohitajika kuendeleza operesheni za amani kwenye maeneo husika UM kwa sasa umepokea ndege sita tu.

Naibu KM kuhusu Masuala ya Kisiasa, B. Lynn Pascoe amewaarifu wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba juhudi za upatanishi za UM zinaendelea kukithiri kwenye sehemu mbalimbali za dunia, katika kipindi cha hivi sasa. Alisema UM umedhamiria kuzifanya huduma za kulinda, kujenga na kudumisha amani kimataifa kuwa ndio msingi wa kazi za Idara ya Masuala ya Kisiasa iliopo Makao Makuu. Mwelekeo huu mpya ndio uliosababisha Idara ya UM juu ya Masuala ya Kisiasa kuamua kuanzisha Kitengo Maalumu cha Usaidizi wa Upatanishi, ambacho kitafungamana kikazi na ile timu ya wataalamu wa upatanishi waliokwishajiandaa kidharura kupelekwa kwenye eneo lolote la dunia penye matatizo.

Ijumatano Alain Le Roy, Naibu KM Mdogo juu ya Operesheni za Amani za UM Duniani ataelekea mji mkuu wa Marekani wa Washington DC kushiriki kwenye sanjari ya mazungumzo ya ngazi za juu na maofisa wa Serikali ya Marekani, ikijumlisha maofisa wa Idara za Mambo ya Nje na Ulinzi, pamoja na wale wanaowakilisha Baraza la Usalama wa Taifa. Kadhalika Le Roy anatazamiwa kukutana na wawakilishi wa taasisi muhimu zisio za kiserikali pamoja na zile taasisi zenye kutayarisha sera za kitaifa.