Skip to main content

Mkutano wa UM kupinga ubaguzi waingia siku ya pili

Mkutano wa UM kupinga ubaguzi waingia siku ya pili

Mkutano wa UM dhidi ya Ubaguzi wa Rangi Duniani unaofanyika mjini Geneva sasa hivi leo umeingia siku ya pili ambapo wawakilishi wa hadhi ya juu wamenedelea na mahojiano yao.

Miongoni mwa wawakilishi wa kutoka Afrika Mashariki, walioshiriki kwenye kikao cha Ijumanne asubuhi, alikuwemo Waziri wa Taifa kwa Masuala ya Nchi za Nje wa Uganda, Oryem Henry Okello. Waziri Okello alikiri kwenye risala yake kuwa ameridhika na muktadha wa warka wa Mkutano, uliopitishwa tarehe 17 Aprili (2009) na ile Kamati ya Matayarisho, warka ambao alisema ulibainisha wizani unaohitajika na mataifa, kijumla, kwenye zile juhudi za pamoja za kusukuma mbele vita dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani. Alisikitika kuwa baadhi ya Mataifa Wanachama yaliamua kususia Mkutano, na Mataifa kadha mengineyo yalitoka kwenye ukumbi wa majadiliano hapo jana. Alitumai ukosefu wa Mataifa hayo machache Mkutanoni ni tukio la muda mfupi, na anatumai pia Mataifa husika yatarejea kujiunga tena na juhudi tukufu za kimataifa za kupiga vita ubaguzi, kote ulimwenguni.