Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Navi Pillay, Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu amepongeza maafikiano yaliokamilishwa, kwa mafanikio, na Kamati ya Matayarisho ya Mkutano wa Mapitio Kuhusu Mwito wa Durban dhidi ya Ubaguzi wa Rangi.

Kamati ilifanikiwa kumaliza kuandika warka wa mswada wa kuzingatiwa, na kupitishwa kwenye kikao kitakachofanyika wiki ijayo Geneva, kujadilia utekelezaji wa Mwito wa Durban wa kupambana na janga la ubaguzi wa rangi, warka ambao uliafikiwa na wajumbe wote wa Kamati ya Matayarisho. Taarifa ya UM imeripoti kwamba kufikia Ijumaa asubuhi watu karibu 3,800 walishajiandikisha rasmi kushiriki kwenye Mkutano wa Mapitio ya Mwito wa Durban, ikijumlisha wakuu 100 ziada watakaongoza Mataifa Wanachama pamoja na wawakilishi 2,500 wa kimataifa wa mashirika yasio ya kiserikali.

Ripoti ya karibuni ya Kundi la Wataalamu juu ya hali katika Cote d'Ivoire imebainisha majeshi ya mgambo, ya binafsi, yaliopo nchini yanaendelea kudhibiti mali ya asili katika maeneo kaskazini. Rasilmali hizi husafirishwa nje kwa biashara kwa kupitia mtandao unaohusisha watendaji wa kienyeji na wale wa kigeni. Ripoti ilithibitisha watendaji wa kigeni ndio wanaowapatia nishati, magari na silaha majeshi ya mgambo husika. Kadhalika ripoti imeashiria mazingira ya amani katika Cote d'Ivoire huenda yakaharibika tena na kufumsha fujo na vurugu, pindi utulivu wa kisiasa utaporomoka na ikiwa masilahi ya kibiashara na uchumi ya baadhi ya makundi yenye nguvu nchini yatapuzwa.

Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura ya Kiutu (OCHA) imeripoti mashirika ya UM yamejumuika, kwa sasa, kusaidia kidharura waathirika wa maafa yaliojiri karibuni kusini mwa Afrika baada ya mafuriko kuua watu 150 katika Angola, Namibia, Bukini na Zambia. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeripotiwa kujihusisha na shughuli za kugawa chakula, maji safi na vifaa vya huduma za msingi katika Angola. Shirika la Afya la WHO linaisaidia Serikali ya Angola kwenye zile juhudi za kufanya makadirio ya mahitaji halisi ya umma ulioathiriwa na mafuriko. Kwa mujibu wa taarifa za OCHA, mafuriko ya kusini mwa Afrika vile vile yameathiri Botswana, Malawi na Msumbiji na inakhofiwa hali huenda ikaharibika zaidi kieneo mnamo miezi ijayo baada ya kunyesha mvua isio ya kawaida, hali ambayo inatabiriwa kuendelea katika siku za usoni.