Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umma wa nchi masikini utafadhiliwa msaada wa tiba rahisi ya malaria

Umma wa nchi masikini utafadhiliwa msaada wa tiba rahisi ya malaria

Kutoka mji wa Oslo, Norway kumeanzishwa rasmi, leo Ijumaa, ushirikiano mpya wa kimataifa wa kuwasaidia mamilioni ya watu wanaogua maradhi ya malaria duniani, hasa wale wanaoishi katika nchi za Asia na mataifa ya Afrika kusini ya Sahara. Mradi huu utawapatia umma huo uwezo wa kumudu dawa za tiba ya malaria, dawa ambazo hunusuru maisha ya mgonjwa, hususan wale watoto wa umri mdogo.

Ushirikiano huu unatarajia, awali, kufadhilia dola milioni 225 zitakazotumiwa kuwapatia, kwa urahisi, umma muhitaji wa nchi masikini dawa ya kupambana na malaria sugu. Bayana hii iliripotiwa na Waziri wa Nchi za Kigeni wa Norway, Jonas Gahr Store, ambaye taifa lake ni miongoni mwa wadau husika wakuu wa mradi huu wa malaria pamoja na mataifa mengine tajiri, yakichanganyika na taasisi nyengine zinashughulikia misaada ya maendeleo.