JKK, Rwanda na UNHCR wajumuika kusailia taratibu za kurudisha makwao wahamiaji
Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti, kwa kupitia msemaji wake mjini Geneva, kuwa na matumaini ya kutia moyo, kufuatia uamuzi uliochukuliwa wiki hii na serikali za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) na Rwanda, wa kukubali kuwasaidia raia waliohamia nchi mbili hiz kurudi makwao, kufuatia misiba kadha wa kadha iliolivamia eneo la Maziwa Makuu katika siku za nyuma.
Maofisa wa Serikali za JKK na Rwanda walikutana kwa siku mbili mjini Goma, kwenye kikao maalumu kilichosimamiwa na UNHCR, ambapo walizingatia hatua, za awali, za kuchukuliwa kitaifa ili kuwawezesha wahamiaji wanaokadiriwa 150,000 kurejea makwao kwa usalama. Kwa mujibu wa taarifa za serikali ya JKK, raia wa Rwanda, wanaokadiriwa 100,000 walikuwa wakiishi katika eneo la Kongo mashariki tangu 1994, kufuatia mauaji ya halaiki yaliotukia Rwanda ambapo jamii ya watu karibu milioni moja waliuawa kutokana na sababu za kijadi. Kadhalika, UNHCR inaripoti raia 53,000 wa Kongo wanaoishi Rwanda, sasa hivi, walianza kumiminikia taifa jirani kuanzia 1996, baada ya mapigano na uhasama sugu kufumka katika jimbo la mashariki la JKK.