Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Huduma za Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limefungua rasmi vituo viwili vya uratibu kwenye miji ya Sake na Kiwanja, iliopo Jimbo la Kaskazini la Kivu, eneo ambalo makundi ya waasi wa Rwanda pamoja na wale wa FDLR bado wanaendelea kuhujumu raia.

Vituo hivi vitatumiwa na majeshi ya Kongo, kuisaidia Serikali kurudisha tena hali ya utulivu na kudhibiti amani kwenye zile sehemu za vurugu na fujo ziliopo kaskazini-mashariki ya nchi.

Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti kuwa na wasiwasi kuhusu hatari ya janga la njaa kuvamia tena umma wa Usomali pindi ile meli ya Sea Horse, iliotekwa nyara tarehe 14 Aprili, haitoachiwa na kuruhusiwa kwenda kupakia shehena ya tani za metriki 7,000 za chakula za kukidhi mahitaji ya wale raia wanaosumbuliwa na njaa Usomali.

Kadhalika, WFP imeripoti bandari ya Mombasa bandari ni muhimu katika kuendesha operesheni za kugawa chakula katika Usomali na kwenye maeneo mengine ya Afrika mashariki na Afrika ya kati. Takwimu za WFP zinaonyesha katika mwaka 2008 zaidi ya tani za metriki 500,000 zilihudumiwa umma muhitaji wa maeneo hayo kwa kupitia bandari ya Mombasa. WFP imeonya pindi misaada ya chakula itashindwa kufikishwa bandarini Mombasa mapema, inahofiwa mamilioni ya watu watasibiwa njaa hatari pamoja na tatizo sugu kuu la utapiamlo, matatizo ambayo yanausumbua umma wa katika sehemu za mataifa ya Usomali, Kenya, Uganda, Sudan kusini na pia katika mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.