Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Liberia imefanikiwa kupunguza madeni iliorithi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe

Liberia imefanikiwa kupunguza madeni iliorithi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe

Liberia imetangaza kuwa imefanikiwa kupunguza, kwa kiwango kikubwa sana, yale madeni inayodaiwa na nchi za kigeni yanayogharamiwa dola bilioni 1.2, baada ya Serikali kuamua kuyanunua madeni ya taifa yaliobakia, kwa bei iliopunguzwa kwa asilimia 97 ya thamani halisi ya madeni hayo.

Makubaliano haya yalikamilishwa baada ya Serikali ya Liberia kulipa dola milioni 38 kwa zile taasisi 25 za kibiashara. Benki Kuu ya Dunia iliisaidia Liberia nusu ya malipo, wakati jumla iliosalia ya madeni ilichangishwa na mataifa ya Ujerumani, Norway, Uingereza na Marekani. Kwa mujibu wa Raisi Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia "mafanikio ya kulipa madeni yaliorithiwa na Serikali yake ni hatua muhimu katika kufufua tena shughuli za maendeleo ya kiuchumi na jamii," kwa kuisahilishia ule mzigo wa madeni ya kigeni ambayo alisema yalipanuka, baada ya kukithiri kwa ushuru wa mikopo na gharama ziada za kuchelewesha malipo ya madeni. Raisi Sirleaf anaamini Liberia, sasa hivi, itavutia mchango maridhawa wa misaada kutoka wawekezaji wa kimataifa, unaohitajika kukuza uchumi na maendeleo ya nchi kwa utulivu unaotakikana kibiashara.