Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji wa Usomali 60,000 warejea Mogadishu

Wahamiaji wa Usomali 60,000 warejea Mogadishu

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti raia 60,000 wamesajiliwa kurejea kwenye mji mkuu wa Usomali wa Mogadishu mnamo miezi mitatu ya mwanzo ya 2009, baada ya hali ya mapigano kupungua.

Asilimia kubwa ya wahamiaji hawa wanarejea makwao kutoka makazi ya muda ya wahamiaji wa ndani (IDPs), yaliopo kwenye maeneo ya kati-kusini na majimbo ya kati ya Usomali. Iliripotiwa mapigano mapya baina ya makundi ya upinzani yenye silaha dhidi ya vikosi vya serikali, yaliofumka Usomali mwezi Machi, yalisababisha watu 1,200 kung'olewa makazi. Kadhalika, UNHCR imeripoti wahamiaji wa KiSomali ziada 2,200 walisajiliwa kurejea nchini mwao kutoka Kenya; 300 kutoka Yemen na 20 walirejea kutoka Ethiopia, wakijumuika pamoja na kundi la wahamiaji 900 ziada wa Usoamli waliowakilisha mchanganyiko wa raia wahamiaji na wale waliofukuzwa nchi kutoka Saudi Arabia. Licha ya kuwa wahamaji raia hawa wa Kisomali wanaonyesha hima kuu nahamasa ya kurudi makwao katika kipindi cha hivi sasa, hata hivyo, UNHCR inahadharisha, huu sio wakati unaofaa kwa wahamiaji wa Kisomali kurejea kwenye mji wa Mogadishu, kwa sababu kuna ukosefu mkubwa wa huduma za msingi na hali ya usalama iliopo kimazingira ni ya kigeugeu.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNHCR wahamiaji wanaorejea Mogadishu sasa hivi hukabiliwa na matatizo kadha wa kadha ya kihali yenye sehemu nyingi, ikijumlisha ukosefu wa makazi. Idadi kubwa ya nyumba ziliopo kwenye maeneo wanaorejelea wahamiaji ziliangamizwa, na kuharibiwa, katika miaka miwili iliopita kwa sababu ya mapigano makali yaliovuma huko wakati huo.

Hivi sasa UNHCR inaongoza mashirika ya UM kwenye zile shughuli za kukadiria hali halisi ilivyo katika mji wa Mogadishu, ili kuashiria bora mahitaji hakika ya kiutu kwa wahamiaji wanaorejea huko. Mashirika ya UM yametangaza nia ya kufungua tena ofisi zao kwenye mji wa Mogadishu, pindi hali ya utulivu, na usalama, itayaruhusu kufanya hivyo.