Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Baraza la Usalama lilifanyisha kikao rasmi Ijumatatu alasiri na kupitisha maafikiano yanayojulikana kama Tamko la Raisi kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea (Korea ya Kaskazini).

Tamko hili la Raisi lilishtumu kitendo cha "urushaji wa chombo angani" na Korea Kaskazini, ambacho kilielezwa kupigwa marufuku kwenye azimio la Baraza la Usalama nambari 1718. KM amekaribisha uamuzi wa Baraza kupitisha Tamko la Raisi hili ambalo anaamini limebainisha dhahiri umoja wa mawazo miongoni mwa jamii ya kimataifa, dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Umma wa Korea. Alitumai ujumbe huu utasaidia kufufua tena zile juhudi za kuleta suluhu ya amani kuhusu masuala yote yanayofungamana na hali katika Ghuba ya Korea, ikijumlisha yale Mazungumzo ya Pande Sita pamoja na majadiliano ya amani kati ya Korea mbili.

Shirika la UM Kusaidia Huduma za Amani katika Afghanistan (UNAMA) limetoa taarifa ilioleza kuchukizwa sana na mauaji ya kihorera yaliotukia Ijumapili, kwenye mji wa Kandahar, dhidi ya mbunge mwanamke wa jimbo aitwaye Sitara Achikzai. UNAMA ilisema mwanabunge Achikzai alikuwa mwanamke jasiri, aliyejitolea kutumikia taifa lake bila ya woga, kwenye eneo la Afghanistan liliopamba fujo na vurugu. UNAMA imelaani vikali mauaji ya Achikzai na kusisitiza waliomwua wameonyesha utovu wa kutojali hishima na mila ya jadi ya Afghanistan.

Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa na wahka mkuu juu ya uamuzi wa wa kutobatilisha ndoa ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka minane uliochukuliwa na mahakama za Saudi Arabia. Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Ann Veneman alinakiliwa akisema kwamba ndoa ya mtoto aliye chini ya umri wa utu uzima, unaokubalika kisheria, ni kitendo kinachoharamisha haki ya mtoto, bila kujali mfumo wa sheria ulivyo katika Saudi Arabia. Uhalali wa idhini ya khiari, ilio huru, kuhusu ndoa, alisisitiza Veneman, ni haki inayotambuliwa na Mwito wa Kimataifa juu ya Haki za Binadamu. Alisema ridhaa ya ndoa haiwezi kuwa halali, huru au ya khiari pindi aliyeahidiwa kuolewa hajatimia umri wa utu uzima wa kufanya uamuzi wenye nguvu ya kisheria.