Skip to main content

Suala la JKK lazingatiwa tena kwenye Baraza la Usalama

Suala la JKK lazingatiwa tena kwenye Baraza la Usalama

Baraza la Usalama leo asubuhi lilikutana kwenye kikao cha hadhara kusailia hali, kwa ujumla, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK).

 Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM katika JKK, na Mkuu wa Shirika la Operesheni za Ulinzi Amani Nchini (MONUC) alielezea maendeleo yaliopatikana hadi sasa katika kurudisha hali ya utulivu na amani, hususan katika eneo la mashariki, ambapo alisema baadhi ya vikundi vya mgambo vimetangaza kuridhia kusimamisha mapigano na kujiunga na na Jeshi la Taifa la Kongo. Wakati huo huo alikumbusha ya kwamba jukumu la kuhifadhi na kuwalinda raia nchini, kwenye eneo lilio kubwa la JKK ni mzigo mzito kwa Shirika la MONUC ambalo halikujaaliwa nyenzo na wala vifaa vya kutosha, vinavyotakikana kutekeleza kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama. Kwa hivyo, aliyataka Mataifa Wanachama kukithirisha mchango wao ili kuiwezesha MONUC kuendeleza operesheni zake nchini Kongo kama inavyosatahiki.