Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Mahakama Maalumu juu ya Makosa ya Vita katika Sierra Leone leo imetoa hukumu kwa viongozi watatu wa kundi la RUF, waliokutikana na makosa ya kushiriki kwenye jinai ya halaiki dhidi ya raia wasiokuwa na hatia. Issa Sesay amehukumiwa kifungo cha miaka 52, Morris Kalon amepewa adhabu ya kifungo cha miaka 40 na Augustine Gbao amehukumiwa kifungo cha miaka 25 kutokana na vitendo viovu, makosa ya vita, jinai dhidi ya utu ikichanganyika na ukatili mwengine uliokiuka sheria ya kiutu ya kimataifa.

Kwenye kikao kisio rasmi cha Baraza Kuu, kilichokutana Ijumanne kwenye Makao Makuu ya UM, KM aliwaelezea wajumbe wa kimataifa matokeo ya safari zake za karibuni, hususan kuhusu ile ziara yake ya London ambapo alihudhuria mkutano wa Mataifa Wanacahama wa Kundi la G-20. Alisema aliingiwa na moyo kuona viongozi wa kimataifa wanashirikiana kwenye juhudi za kuchukua hatua halisi kutatua mgogoro wa uchumi duniani, kwa lengo la kutunza ustawi na hali njema kwa umma wa dunia. KMalitumai ahadi zilizotolewa London zitatekelezwa kwa vitendo na sio kauli pekee.

Rodolphe Adada, Mpatanishi Maalumu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur aliokutana Ijumatano na Minni Minawi, aliye Msaidizi Maalumu wa Raisi wa Sudan na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mpito ya Jimbo la Darfur na walizungumzia masuala kadha, ikijumlisha taratibu za kuimarisha usalama na hali ya kiutu katika Darfur pamoja na masula yanayoambatana na huduma za maendeleo ya kiuchumi na jamii.