Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa kimataifa wathibitisha nishati anuwai ya viumbehai inahitajika kukuza maendeleo vijijini

Wataalamu wa kimataifa wathibitisha nishati anuwai ya viumbehai inahitajika kukuza maendeleo vijijini

Ripoti mpya kuhusu matokeo ya utafiti wa kimataifa juu ya matumizi ya nishati kwa wanavijiji, iliotolewa wiki hii, na kuchapishwa bia na Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na Idara ya Uingereza Inayohusika na Maendeleo Kimataifa (DFID) imethibitisha ya kuwa pindi uzalishaji wa japo kiwango kidogo cha nishati kutoka anuwai ya viumbehai utatekelezewa jamii za kienyeji, kadhia hiyo ina matumaini ya kuimarisha, kwa kiwango kikubwa, shughuli za maendeleo vijijini, hasa katika nchi masikini.

Mada ya utafiti huo inasema: "Mpango wa Nishati ya Viumbeanuwai: Maelezo Mafupi na Mafunzo ya Awali juu ya Athari kwenye Tartibu za Kupata Riziki Baada ya Uchunguzi Uliofanyika Amerika ya Latina, Asia na Afrika". Utafiti uliendelezwa kwenye miradi 15 inayotumia teknolojia kadha wa kadha za kuzalisha nishati inayotokana na anuwai ya viumbehai, miradi ambayo ilianzishwa kwenye nchi 12 za Afrika, Amerika ya Latina na Asia. Mathalan, utafiti umegundua nishati inaweza kuzalishwa, kwa ufanisi na umadhubuti, kutoka takataka ambazo mara nyingi hutupwa ovyo na huwachwa kuoza. Kadhalika utafiti wa wataalamu wa kimataifa umethibitisha uzalishaji wa gesi inayotokana na viumbehai hufanya pia mbolea kutoka mabaki ya kadhi hiyo. Wataalamu wanaamini, halkadhalika, utaratibu wa kutengeneza nishati ya viumbeanuwai una uwezo wa kuzalisha, kwa pamoja, chakula na nishati kwa kutumia kilimo mseto. Kadhia hizi na huduma kadha nyenginezo kama hizo zikitekelezwa hufaidisha jamii nyingi za kienyeji na huwawezesha kupata nishati, kwa urahisi, kwa matumizi ya majumbani na pia kwenye shughuli za kibiashara.