Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

B. Lynn Pascoe, Naibu KM juu ya Masuala ya Kisiasa aliwasilisha, asubuhi, kwenye kikao cha faragha cha Baraza la Usalama, ripoti fafanuzi kuhusu hali ya wasiwasi iliojiri baina ya mataifa ya Djibouti na Eritrea. Kadhalika Pascoe aliwakilisha taarifa kuhusu mtafaruku wa kisiasa uliojiri Bukini mnamo wiki za karibuni. Baada ya mashauriano ziada miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Usalama, kuliitishwa kikao rasmi kingine cha kuzingatia hali katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Taarifa ya Raisi wa Baraza la Usalama, iliopitishwa kufuatia kikao hicho, imevisihi vile vikundi vyenye silaha nchini kukomesha haraka fujo. Taarifa pila iliyahadharishab makundi hayo yenye silaha kuwacha tabia ovu ya kuajiri watoto wadogo, ambao huwalazimisha kushiriki kwenye vita na mapigano.

Mashirika sita ya UM yaliopo Bukini, yakichanganyika na jumuiya tatu za kiraia, yameanzisha kampeni maalumu yenye maombi ya kutaka yafadhiliwe msaada wa dola milioni 35.7 ili kudhibiti uchakavu, pamoja na uharibifu wa hali ya kiutu uliozuka nchini katika mwaka huu. Mnamo 2009 Bukini ilishuhudia mizozo kadha wa kadha, iliojumlisha ukame, vimbunga na pia kipindi cha fujo za kisiasa. Idadi ya umma utakaohitaji kusaidiwa kihali kutokana na msaada huo inakadiriwa kufikia milioni 2.5, na wingi wa umma huu huishi katika miji. Kadhalika watu 880,000 wengine wanaoishi kusini, kwenye yale maeneo yaliodhuriwa na ukame nao pia watahitajia msaada wa kimataifa ioli kukidhi maisha.

Mapigano yaliofumka tena kwenye wilaya ya Ituri, katika mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), baina ya makundi mawili ya mgambo, yamesababisha watu 30,000 kung'olewa makazi, kutokana na ripoti iliotolewa na Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) Ijumanne kuhusu hali katika JKK. Wanavijiji hawa wote sasa hivi wamehamishwa kilomita 50-70 kusini ya Bunia ili kupatiwa usalama na hifadhi bora.

Kadhalika, UNHCR imeripoti tukio la ajali ya wahamiaji waliozama kwenye mwambao wa Yemen. UNHCR ilisema mnamo mwisho wa wiki iliopita watu wanane walizama na watu 22 wengine walipotea, na wanakhofiwa walifariki katika Ghuba ya Aden, baada ya kuwachwa na wafanya magendo nje ya mwambao wa Yemen. Takwimu za UNHCR zinaonyesha tangu mwanzo wa mwaka 2009 mashua 339 zilisajiliwa kuwasili Yemen kimagendo, na zilibeba abiria 17,000 waliotokea mataifa ya Pembe ya Afrika, abiria waliovushwa na wafanya magendo kwenye bahari hatari ya Ghuba ya Aden. Asilimia kubwa ya umma huu huhajiri makwao ili kuepukana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini, pamoja na kukwepa hali ya wasiwasi wa kisiasa, ufukara na matatizo ya njaa, hususan katika taifa la Usomali. UNHCR imeripoti watu 74 walisajiliwa kufariki tangu mwanzo wa mwaka kwa sababu ya safari za magendo na watu 51 wengineo waliripotiwa kupotea.