Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya Afya Bora Duniani kwa 2009

Siku ya Afya Bora Duniani kwa 2009

Tarehe ya Aprili 07, huadhimishwa kila mwaka na UM kuwa ni Siku ya Afya Bora Duniani. Mwaka huu kumetolewa mwito maalumu na UM unaozihimiza serikali za kimataifa, kuwekeza zaidi kwenye mahospitali na kwenye vifaa na nyenzo nyengine za kutunza afya, vifaa ambavyo ni muhimu sana katika kuokoa maisha ya umma wenye kuathirika na matatizo ya kiutu.

 Risala ya KM Ban Ki-moon, katika kuiadhimisha Siku ya Afya Bora Duniani ilikumbusha kuwa "maafa yanapopiga mahali, awali ni huduma za afya, zilizotayarishwa vizuri, na zinazofanya kazi kama zinavyotakiwa, zinazopewa umbele." Mada ya kampeni ya Siku ya Afya Duniani kwa 2009 inasema "Ukitaka kuokoa maisha ya umma kwenye maafa ya kimaumbile, au kiutu, hakikisha hospitali zinakuwa salama kwenye mazingira ya dharura." Dktr Margaret Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani alitanabahisha fafanuzi za "kustaajabisha" kwenye risala yake ya kuiadhimisha Siku ya Afya Duniani. Alisema wataalamu wa kimataifa wamethibitisha, kihakika, kwamba gharama za ujenzi wa hospitali zinazovumulia mitikisiko ya pepo kali, na kusthamaili mafuriko, au matetemeko ya ardhi ni "ndogo sana". Kwa hivyo, WHO imezihimiza serikali wanachama, wahudumia afya, jumuiya za kiraia, pamoja na wafadhili wa kimataifa na umma, kwa ujumla, kufanya kila wawezalo kuchangisha matayarisho bora kwenye sekta ya afya, yatakayowawezesha kukabiliana vyema pale hali ya dharura inapojiri kwenye maeneo yao. Lengo la nasaha hii hasa ni kuhakikisha nyenzo za afya - kama vile mahospitali, vituo vya huduma za afya ya msingi, zahanati ndogo ndogo na taasisi nyengineo kama hizo - huwa zinakamilishiwa uwezo bora wa kuhimili kazi zake inapojiri hali ya dharura na baada ya maafa kumalizika, mathalan, fujo na vurugu, au tetemeko la ardhi na vimbunga.