Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Taarifa iliotolewa na Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) imeeleza tishio la uharamia nje ya mwambao wa Usomali, ni tukio la kila siku, hali ambayo ilisababisha ucheleweshaji mkubwa katika kupeleka misaada ya chakula Usomali, na kwenye maeneo mengine ya Afrika mashariki na Afrika ya kati. Kwa mujibu wa taarifa ya WFP, meli ya Kimarekani ya kampuni ya Maersk Alabama, iliotekwa nyara wiki iliopita kwenye mwambao wa Usomali, ilikuwa imebeba shehena ya makontena 232 ya msaada wa chakula, uliojumlisha pia tani 4,000 za lishe ya kutibu utapiamlo kwa mama na watoto wa Afrika mashariki na kati. Meli ya Maersk Alabama, iliokuwa ikielekwa bandari ya Mombasa, Kenya ilikuwa imechukua msaada wa chakula uliokusudiwa kuhudumia watu milioni 8 walioathirika na ukame pamoja na bei ghali ya chakula katika mwaka huu kwenye maeneo ya Usomali, Kenya na Uganda.

Imeripotiwa kutoka Geneva ya kuwa ile tume iliodhaminiwa madaraka ya kutayarisha ajenda ya Mkutano wa Durban juu ya Mapitio ya Juhudi za Kudhibiti Ubaguzi wa Rangi Ulimwenguni inakaribia kumaliza kuandika nakala ya mwisho ya mswada wa ajenda ya mkutano. Vile vile ripoti pia imeeleza mashirika yasio ya kiserikali 250 yameshasajiliwa, kwa sasa, kuwa yatahudhuria Mkutano wa Durban, na inatumainiwa idadi hiyo itabadilika kila tukikaribia siku ya kufunguliwa mkutano wiki ijayo.