Ban atowa mwito wa msaada zaidi kwa juhudi za kupambana na UKIMWI, TB NA Malaria

Ban atowa mwito wa msaada zaidi kwa juhudi za kupambana na UKIMWI, TB NA Malaria

Katika wakati huu wa misukosuko ya kiuchumi, kugharimia vita dhidi ya UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria ni uwekezaji wa busara, alisema KM Ban Ki-moon hii leo alipowahimiza wafadhili kugharimia juhudi za UM kuzuia kuenea kwa magonjwa hayo ya hatari.

Katika ujumbe wake wa video kwa mkutano wa kati ya mwaka, kutathmini kugharimia kwa hiyari Fuko la Kimataifa la kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria, Global Fund, Bw Ban alionya kwamba, kote barani Afrika UKIMWI unatishia kupunguza mapato ya wastani ya taifa GDP kwa hadi asili mia 2.6. Bw Ban alidokeza kwamba tangu 2001 Global Fund, imetumia zaidi ya dola bilioni 10 kwa ajili ya miradi ya afya katika mataifa 140 duniani. Baada ya ujumbe huo KM aliwahutubia viongozi wa Umoja wa Nchi za Kiarabu waloanza mkutano wao huko Doha Qatar, akieleza wasi wasi wake kuhusiana na hali ya Gaza, na kutoa mwito kwa viongozi hao kusaidia katika kupatikana suluhisho kati ya Israel na Palestina. Alisema wakazi wa Gaza wanataabika na hali katika vituo vya kuvuka mpaka siya kukubalika. Alisema njia kuelekea mbele, ni kupatikana usitishaji mapigano kwa kudumu, upatanishi wa wa-Falestina chini ya Rais Mahmoud Abass. Amesema, serekali mpya ya Israel inalazimika kuwaruhusu wakazi na bidhaa za wa-Falestina kusafiri kwa uhuru, na lazima kusitisha ujenzi wowote wa makazi ya wayahudi, na kusitisha kujichukulia hatua za kipekee huko Jerusalem na kuendelea na majadiliano. Katika hotuba yake Bw Ban alizungumzia maendeleo ya huko Somalia, pamoja na wasi wasi wake wa hali ya maisha huko Darfur hasa baada ya kufukuzwa mashirika 13 ya misaada, na maendeleo ya kisiasa Lebanon na Irak.