Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon amewahimiza watu wote kuungana na UM na mamilioni ya watu kote duniani kupeleka ujumbe kwa viongozi wa serekali zao kulinda mazingira ya Dunia kwa kuzima taa kwa saa moja Jumamosi usiku.

Mjumbe maalumu wa UM kwa ajili ya Somalia Ahmedou Ould-Abdallah amelaani vikali walohusika na mripuko wa bomu lililotegwa kando ya barabara, mripuko ulosababisha kujeruhiwa waziri wa mambo ya ndani wa Somalia Sheikh Abdulkadir Ali Omar na kuuliwa mmoja wa washauri wake. Bw Ould-Abdallah alisema alishtushwa na shambulio hilo dhidi ya waziri aliyekua anatembea pamoja na washauri wake katika soko mashuhuri lililokua limejaa watu la Bakara huko Mogadishu. Amesema utawala mpya wa Rais Sharif Sheikh Ahmed unafanya juhudi za kuimarisha usalama, kupata rasilmali na kuwasaidia wa Somali kurudi katika maisha ya kawaida kama katika nchi nyenginezo za Afrika.

Akikutana na waziri wa mambo ya nchi za njee wa Pakistan Makhdoom Shah Qureshi, KM alisema amechukiszwa na shambulio la bomu la Ijumaa kwenye mskiti mmoja kaskazini magharibi ya Pakistan na kutoa rambi rambi kwa familia za waathiriwa. Kiasi ya watu 50 wanaripotiwa wameuliwa na wengine wengi kujeruhiwa wakati wa swala ya Ijumaa. Bw Ban alisema Pakistan ina jukumu muhimu kabisa katika utaratibu wa amani ya Afghansitan, na suluhisho la kijeshi pekee halitoshi kuleta utulivu bila ya kuimarisha juhudi za kisiasa na kiuchumi.