Ban anasema mataifa yanayoendelea yanahitaji dola trilioni
KM wa UM Ban Ki-moon amewambia viongozi wa mataifa tajiri kabla ya mkutano wa G20 kwamba, mataifa yanayoendelea yanahitaji dola trillion moja kuweza kukabiliana na mzozo mkubwa wa fedha duniani.
Alisema hadi pale hatua za dharura na thabiti zinachukuliwa kupunguza athari za kudumaa uchumi wa dunia, mzozo huo utazorota zaidi kwa kukumbwa pia na ukosefu uthabiti kote duniani. Bw Ban alieleza hayo katika barua iliyotolewa jana kwa viongozi wa kundi la mataifa 20 tajiri na inayoinukia, G 20, wanaotazamiwa kukutana mwezi ujao huko London. Alitoa mwito wa kuchukuliwa mkakati wa ncha nne ili kuzuia kuzuka maafa mepya, kwa kuanza na mpango wa dhati wa kuchochea uchumi wa dunia nzima, utakaokidhi mahitaji ya mataifa yanayoendelea pia. KM aliwahimiza viongozi wa G20 kuendelea kugharimia miradi ya UM na Benki Kuu ya Dunia ili kuwawezesha kujibu mzozo huo kwa namna inavyostahiki.