Skip to main content

UNHCR - Wasomali wazidi kukimbilia Kenya

UNHCR - Wasomali wazidi kukimbilia Kenya

Maelfu ya wa Somali wanaendelea kukimbilia kaskazini mashariki ya Kenya kutafuta hifadhi katika makambi ya wakimbizi yaliyofurika watu ya Dadaab, licha ya kuwepo na serekali mpya Mogadishu na kupunguka kwa ghasia nchini humo.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, kufuatana na Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR, wakimbizi wepya elfu 20 wameandikishwa katika makambi matatu jirani ya Dadaab. Wengi wa wakimbizi wepya waliohojiwa na UNHCR wanataja kuongezeka hali ya ukosefu wa usalama hasa katika maeneo ya kati na kusini ya Juba, pamoja na ukame na upungufu wa chakula kama sababu za kukimbilia Kenya. Kambi za Dadaab zilijengwa miaka 20 iliyopita, ili kuweza kuwapokea watu elfu 90, lakini hii leo ni makazi ya zaidi ya watu elfu 261.

Wakati huo huo UNHCR inaripoti kwamba ina wasi wasi mkubwa kutokana na hatima ya maelfu ya raia walokimbuia makazi yao kutokana na mashambulio ya kila siku ya makundi yenye silaha huko kaskazini mashariki ya JKK. Tume ya kutathamini hali ya mambo ya UM iliyotembelea eneo hilo wiki hii imeripoti kwamba, wanamgambo wa kundi la FDLR wa Rwanda na washirika wao PARECO wamekizingira kijiji cha Pinga, Kivu ya Kaskazini na kusababisha hofu miongoni mwa wakazi 8 500 wa kijiji hicho pamoja na watu 2 000 walokimbia makazi yao kabla na kuishi katika kijiji hicho.

Kwa upande mwengine inaripotiwa kuna zaidi ya watu elfu 20 wamekimbia kutoka vijiji vitatu vya wilaya ya Rutshuru, Kivu ya Kaskazini baada ya kushambuliwa na makundi yenye silaha mnamo wiki chache zilizopita.