Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mvua kali ya tishia mafuriko zaidi huko Namibia na Angola

Mvua kali ya tishia mafuriko zaidi huko Namibia na Angola

Idara ya Huduma za Dharura ya UM OCHA, inasema mafuriko yanayotokea huko Namibia na Angola kutokana na mvua kali za wiki tano zilizopita yanahatarisha kueneza magonjwa ya kipindupindu na malaria.

Msemaji wa OCHA mjini Geneva Elizabeth Byrs anasema hadi hivi sasa hawana idadi halisi ya waloathirika hata hiyo kuna watu 92 walofariki na watu laki mbili zaidi wamepoteza makazi yao ambapo kiasi ya 8 200 wamewekwa katika makambi ya muda.

"Timu mbili za watalamu kutoka mashirika ya misaada zimepelekwa katika maeneo yaliyoathirika kutathmini hali ya mambo na moja tayari imeripoti juu ya matatizo ya ukosefu wa maji masafi, huduma za afya, na kutoa uchafu pamoja na chakula kwa sababu maeneo makubwa ya mashamba yameharibika."

Rais Pohamba alitangaza hali ya hatari na kusema kutokana na kuharibika kwa hekta chungu nzima za ardhi kutakuwepo na tatizo la chakula na alitoa mwito kwa msaada wa Kimataifa. Bi Byrs anasema hadi hivi sasa hawajapokea rasmi ombi la msaada, hata hivyo kuna timu ya msaada iliyotayari kuelekea huko itakapopata mwaliko.