Skip to main content

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon amezihimiza pande zote huko Madagascar kuhakikisha utulivu na mpito makini wa kidemokrasia kufuatia kujiuzulu kwa Rais Marc Ravalomanana.

Kikosi cha pamoja cha UM na AU huko Darfur UNAMID, kimelaani vikali shambulio la kuvizian Ijumanne asubuhi lililosababisha kifo cha mlinda amani mmoja, katika mji wa Nyala mji kuu wa jimbo la Darfur ya kusini. Hilo lilikua shambulio la pili dhidi ya walinda amani mnamo wiki moja, na UNAMID imetoa mwito kwa pande zote zinazohusika pamoja na serekali ya Sudan kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa UM katika eneo hilo.

Idara ya kuratibu huduma za dharura ya UM OCHA imetangaza hii leo kwamba wakazi walokimbia makazi yao huko kaskazini ya Uganda kutokana na mapigano ya miongo miwili kati ya majeshi ya serekali na kundi la waasi wanaendelea kurudi nyumbani. Mapigano kati ya majeshi ya serekali ya Uganda na waasi wa Lord's Resistance Army yamesababisha karibu watu milioni mbili kukimbia makazi yao, kuharibu miundo mbinu na huduma muhimu. OCHA inaeleza kwamba tangu Disemba 2008 karibu watu elfu 80 wamesharudi katika vijiji vyao huko Uganda kutoka kwa makambi au vituo vya muda.