Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon akifuatana na rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton wako Haiti hii leo ili kuhamasisha dunia nzima juu ya mahitaji ya kukarabati na kuufufua uchumi wa taifa hilo la Caribbean.

Wakati wa ziara yao ujumbe wa KM utatembelea miradi ya elimu katika kitongoji maskini kabisa cha Cite Soleil, na kukutana na rais Rene Preval, maafisa wa serekali, jamii ya wafanyabiashara na mashirika yasio ya kiserekali. Baada ya ziara hiyo Bw Ban atafika Washington Jumanne kukutana na Rais Barack Obama kwa mazungumzo juu ya masuala mbali mbali ya kimataifa. Benki Kuu ya dunia yamesema mataifa yanayoendelea yatakabiliwa na upungufu wa dola bilioni 700 mwaka huu kutokana na mzozo wa kifedha na hasa utoaji mikopo duniani. Rais wa Benki Kuu Robert Zollick, alisema mzozo wa dunia unahitaji suluhisho la kimataifa na ili kuzuia kutokea janga la kiuchumi katika mataifa yanayoendelea, ni muhimu kuwepo na juhudi ya kimataifa kukabiliana na mzozo huo. Maelezo hayo yametolewa leo kabla ya mkutano wa mataifa tajiri na yanaoinukia ya kundi la G20 huko London.

Mratibu wa Huduma za Dharura wa UM John Holmes amesema, UM unafanya kila njia kujaribu kubadilisha amri ya serekali ya Khartoum ya kuyafukuza makundi 13 muhimu ya misaada ya dharura kutoka jimbo lenye ghasia la Sudan la Darfur. Wakati huo huo mipango inaendelea kujaribu kuziba mwanya uloachwa kutokana na kufukuzwa mashirika hayo yaliyokua yanatoa msaada wa kuokoa maisha kwa karibu wa-Sudan milioni 4.7 walokimbia makazi yao. Bw Holmes aliwaambia wandishi habari mjini New York kwamba, wamekua wakiwasiliana na serekali ya Sudan katika viwango mbali mbali pamoja na wadau wengine wamekua wakifanya hivyo mwishoni mwa wiki, na amesema hata ikiwezekana majadiliano kati ya Rais Bashir na Bw Ban, kwa wakati muafaka yatapangwa.