Hapa na pale

Hapa na pale

Mjumbe Maalum wa UM huko JKK, Alan Doss amesema, ili kukomesha udhalilishaji na utumiaji nguvu wa ngono uloenea huko mashariki ya Kongo, ni lazima kusitisha shughuli za makundi yenye silaha, lakini pia kuhakikisha vikosi vya usalama vina nidhamu kamili.

Akijibu masuali ya kundi la wanawake waloathiriwa na vitendo vya utumiaji nguvu, anapoendelea kutathmini hali ya kibinadamu huko jimbo la Kivu ya kaskazini Bw Doss alisistiza haja ya kukomesha kuwepo na makundi yenye silaha, lakini lazima pia kuvifunza nidhamu na adabu vikosi vya usalama. Baraza la Usalama limeiomba ofisi ya UM huko DRC MONUC kuweka kipaumbele chake kua, ni kuleta utulivu katika majimbo ya mashariki na usalama wa raia.

Akieleza hali ya usalama ya Liberia kua imara kwa hivi sasa, lakini mwakilishi wa UM nchini humo anaonya kwamba kuna changamoto muhimu zilizobaki katika sekta za usalama na utawala wa sheria. Akizungumza kwenye kikao cha faragha cha Baraza la Usalama kuwasilisha ripoti mpya ya KM juu ya kazi za afisi yake huko Liberia UNMIL, Bi Ellen Margrethe alitoa mwito wa msaada thabiti wa jumuia ya kimataifa kusaidia Liberia inapo endelea kujikomboa kutoka vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 14. Alisisitiza kwamba ingawa Liberia si taifa lililoshinda kujitawala tena, lakini nchi iko katika hali tete na katika kanda ambayo bado haina uthabiti.

Akiliarifu Baraza la Usalama juu ya hali huko Afghanistan, mjumbe maalum wa KM Kai Eide amesema, ingawa vipaumbele vya kimataifa huko Afghanistan, ikiwa ni pamoja na usalama, mpango wa muda mrefu wa kuimarisha vyombo vya serekali na uthabiti wakati wote wa uchaguzi ujao vimebaki kua muhimu, lakini kinachokosekana ni rasilmali ya kutosha na nia dhati ya kisiasa. Alisema mkutano ujao juu ya Afghanistan huko The Hague, utatoa nafasi ya kuwepo na nguvu mpya na utayarifu wa pamoja na wala si kutathmini upya vipau mbele vilivyokwisha kubaliwa, bali kua tayari kuvitekeleza na kutumia rasilmali kwa urahisi zaidi na njia ya ushirikiano mkubwa.