Skip to main content

KM analaani vikali mauwaji huko Guinea Bissau

KM analaani vikali mauwaji huko Guinea Bissau

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa matamshi makali kabisa limelaani mauwaji ya rais wa Guinea Bissau Bernardo Vieira na mkuu wake wa majeshi Tagme Na Waie, na kutoa mwito kwa wananchi, viongozi wa kisiasa na majeshi ya nchi hiyo kubaki makini, kujizuia na kudumisha utulivu. Akisoma taarifa ya baraza hilo balozi wa Libya Ibrahim Dabbashi, ambae ni mwenyekiti wa mwezi huu wa baraza hilo amehimiza kwa pande zote nchini humo kutanzua ugomvi wao kupitia mfumo wa taasisi za kidemokrasia na kupinga jaribiyo lolote la kubadilisha serekali kinyume cha katiba.

KM Ban Ki-moon alitoa taarifa yake pia kulaani mauwaji ya viongozi hao na kuvitaka vikosi vya usalama vya nchi hiyo kudumisha utawala wa sheria na kuwafikisha walohusika mahakamani. Umoja wa Afrika na Jumuia ya uchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS, zimelaani pia mauwaji hayo. Spika wa bunge Ramiundo Perreira ameapishwa kua rais wa mpito hii leo na ametoa mwito kwa wananchi wake kusaidia kurudisha utulivu katika taifa hilo ambalo limeshuhudia misukosuko mingi hivi karibuni.