KM anasema, amani ya kudumu ni lazima iwe msingi wa kuikarabati Ghaza

2 Machi 2009

KM wa UM Ban Ki-moon ametoa mwito kwa wafadhili wa kimataifa kutoa fedha zinazohitajika sana kwa ajili ya kazi za kuikarabati Ghaza kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel. Bw Ban alisisitiza kwa mara nyingine tena haja ya kupatikana makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano na makubaliano jumla ya amani.

KM alitoa mwito wa kutaka hatua kuchukuliwa alipokua anahutubia mkutano wa kimataifa juu ya uchumi wa Palestina na kazi za kuikarabati Ghaza katika mji wa mapumziko wa Misri wa Sharm el-Sheik. Israel ilifanya mashambulizi ya wiki tatu kuanzia Disemba 27 mwaka jana kwa lengo la kujibu mashambulio ya roketi ya Hamas na makundi mengine. Kiasi ya Wapalestina 1300 waliuliwa na wengine elfu 5300 walijeruhiwa. Bw Ban aliwahimiza wafadhili kuwa wakarimu katika kusaidia kazi za kukarabati eneo hilo la Ghaza, akisisitiza kwamba wakazi wa Ghaza hawawezi na haijabidi wasubiri kwa muda mrefu zaidi. KM ana maliza ziara yake ya nchi tano za Afrika huko Misri. Hapo jana aliwatembelea wanawake na wasichana waloathiriwa na ghasia za ngono huko mashariki ya JKK. Kufuatana na shirika la UM la watoto UNICEF, kiasi ya wanawake laki mbili walibakwa mnamo mika 12 ya ghasia katika eneo hilo. Akiwa huko Tanzania bw Ban alisema Tanzania ni mfano mzuri wa kuigwa kukabiliana na change moto za afrika katika masuala ya demokrasia, utulivu na elimu. Alikutana na Marais Joseph Kabila wa JKK na Paul Kagame wa Rwanda na kusifu kuimarishwa uhusiano kati ya nchi zao mbili. Alianza ziara yake ya Afrika kwa kuitembelea Afrika Kusini ambako alizungumzia jukumu la nchi hiyo katika kusaidia kuleta amani barani Afrika.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter