Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za UM kudhibiti mazingira bora

Juhudi za UM kudhibiti mazingira bora

Mkutano wa siku tatu kuhusu uchukuzi wa baharini, uliotayarishwa na Shirika la UM juu ya Biashara na Maendeleo (UNCTAD), umehitimisha mijadala wiki hii mjini Geneva kwa mwito uliohimiza wenye viwanda kuhakikisha wanaongeza juhudi zaidi kwenye ile kadhia ya kupunguza umwagaji wa hewa chafu angani.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkutanoni, shughuli za usafiri wa baharini ni moja ya huduma zenye kuathiri mazingira na hujumuisha asilimia nne ya hewa chafu inayomwagwa angani katika dunia. Inakhofiwa pindi tatizo hili haltadhibitiwa mapema inaashiriwa jumla hiyo itaongezeka mara tatu ya kiwango cha sasa itakapotimu 2050. Wataalamu waliohudhuria mkutano wa Geneva walipendekeza miundo ya vyombo vya baharini irekibishwe ili ilingane na mapendekezo ya kudhibiti bora matatizo hayo. Vile vile wataalamu walitaka marekibisho yafanyike kwenye injini za meli na katika namna zinavyotumia nishati.

Kwenye kikao chengine kilichoandaliwa Beijing, kwa sehemu, na Shirika la UM la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) majadiliano yaliofanyika huko yalilenga zaidi kwenye taratibu za kukabiliana namatatizo ya ukame mkali ulionekana kufumka mara kwa mara duniani katika miaka ya karibuni, janga ambalo huchanganyika na hali mbaya ya hewa iliyokiuka mipaka. Baadhi ya wataalamu wa kwenye mkutano walitoa mfamo wa hali hiyo kujiri hivi sasa katika taifa la Australia ambapo kumezuka karibuni hali mbaya ya joto, ikichanganyika na ukame haribifu na moto wa kasi kuu.

Kadhalika, mji wa Copenhagen umesajiliwa rasmi Alkhamisi kuwa ni mshiriki wa 100 wa ushirikiano unaojulikana kwa umaarufu kama Mtandao wa Mazingira ya Hali ya Hewa Huru, ambao huongozwa na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP). Mwaka mmoja uliopita Mtandao wa Mazingira ya Hali ya Hewa Huru ulianzishwa rasmi kimataifa, kwa madhumuni halisi ya kukuza shughuli maalumu zitakazohakikisha umma wa kimataifa utaishi kwenye jamii zenye uchumi usiosumbuliwa na mazingira yaliopambwa na hewa chafu.