Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM ajiandaa kuzuru mataifa matano Afrika

KM ajiandaa kuzuru mataifa matano Afrika

Ofisi ya msemaji wa KM imetangaza kwamba kuanzia wiki ijayo KM Ban Ki-moon atafanya ziara ya kuyatembelea mataifa matano barani Afrika, ikijumuisha Afrika Kusini, Tanzania, JKK, Rwanda na Misri.

Kuhusu Afrika Kusini na Tanzania hii itakuwa ni ziara rasmi ya kwanza ya KM kwenye maeneo hayo, ambapo anatazamiwa kufanya mazungumzo kuhusu masuala ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Atakapokuwa Afrika Kusini KM atakutana na Raisi Kgalema Motlanthe, pamoja na Mawaziri wa Fedha na Mazingira, na vile vile atakutana na Raisi mstaafu Nelson Mandela. Kwenye ziara ya Tanzania KM atafanya mazungumzo na Raisi Jakaya Kikwete, na anatazamiwa kuwahutubia wanadiplomasiya na wanataaluma, atakapokuwepo jijini Dar es Salaam. Kadhalika, KM atazuru Zanzibar ambapo anatazamiwa kufungua rasmi Ofisi ya Kituo Kimoja cha Mashirika ya UM kisiwani huko. Tanzania ni moja ya mataifa kadha yanayoendelea yalioshiriki kwenye ule mradi wa kuunganisha mashirika ya UM yanayohudumia misaada ya maendeleo, chini ya kituo kimoja cha ofisi, mfumo ambao hujulikana kwa umaarufu kama Mradi wa UM Moja. Wakati KM atakapoelekea Arusha kuzuru Mahakama ya Kimataifa juu ya Rwanda (ICTR), ndege yake itaruka juu ya kilele cha Mlima Kilimanajaro ili kumpatia fursa kujionea mwenyewe athari za mabadiliko ya hali ya hewa ambazo zilisababisha theluji na barafu kuyeyuka kwa kasi kileleni.