Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

Mjumbe Binafsi wa KM kwa Sahara ya Magharibi, Christopher Ross, anaelekea kwenye eneo husika kwa ushauri, baada ya kukutana na KM, wajumbe wa Baraza la Usalama na wawakilishi wa makundi husika – yaani, Chama cha Ukombozi wa Sahara Magharibi (Frente Polisario) na Morocco. Ross ataanza ziara yake ya mashauriano kesho Ijumatano katika mji wa Rabat, Morocco. Hii itakuwa ni ziara ya awali kwenye eneo, baada ya kushika rasmi wadhifa wa Mjumbe Binafsi wa KM.

Hapa na Pale

KM ameyakaribisha "Maafikiano ya kujenga hali ya kuaminiana kusuluhisha tatizo la Darfur" yaliotiwa sahihi, Ijumanne ya leo, katika mji wa Doha, Qatar, baina ya wawakilishi wa Serikali ya Sudan na wale wa kutoka kundi la waasi la JEM, chini ya uongozi wa Serikali ya Qatar pamoja na Mpatanishi Mkuu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur, Djibrill Bassolé. Alisema Mapatano hayo yanawakilisha hatua ya kusaidia juhudi za yale mazungumzo ya kurudisha amani kwenye mzozo ulioselelea kwa muda mrefu kwenye eneo husika. KM alisema bila ya makundi yanayohasimiana, kuahidi kuacha vurugu, hali ya amani katika Darfur itaendelea kuzorotoa. Alisisitiza, UM utajitahidi kama iwezavyo kujishirikisha kwenye huduma zote za upatanishi, na katika ulinzi wa amani ya eneo, na kuendeleza shughuli zake bila upendeleo, wakati itahakikisha makundi husika na mzozo wa Darfur yatafikia suluhu ya kisiasa itakayodumisha amani kwenye taifa lao.

   Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) wiki hii vilituma timu maalumu ya uchunguzi kwenye mji wa Wada'ah, Darfur Kaskazini, iliyoongozwa na Kamanda Mkuu, Jenerali Martin Luther Agwai, baada ya kupata ripoti ya kuzuka mapigano ya siku kadha baina ya vikosi vha Serikali ya Sudan na makundi yenye silaha kwenye eneo hilo. Timu ya UNAMID ilipofika Wada'ah walishuhudia uharibifu mkubwa uliofanyika wa majengo kadha, pamoja na uharibifu wa vifaa, majumba, maduka, vibanda na pia majenereta, vitu ambayo viliteketezwa, na mali za marikiti zilinyanganywa, wakati maghala ya nafaka yaliunguzwa moto, na majivu yake yalionekana yakifukuta moto. Kadhalika, wawakilishi wa timu ya UNAMID walichukuliwa kuzuru sehemu mbili zilizopo kwenye vitongoji vya Wada'ah, na huko walishuhudia matuta ya udongo mbichi, yaliowakilisha makaburi ya watu 45 waliozikwa hapo, kwa mujibu wa taarifa ya wenyeji waliosema wana ushahidi hakika wa tukio hilo. Halkadhalika, wenyeji wanasema idadi kubwa ya watu waliokimbia mapigano hawajulikani walipo.

   Kadhalika, ripoti ya karibuni ya KM kuhusu watoto walionaswa kwenye mazingira ya fujo na vurugu Sudan, iliotumiwa Baraza la Usalama, ripoti imebainisha watoto wenye umri mdogo bado wanaajiriwa, kimabavu, na kutumiwa kwenye mapigano na makundi yote yanayohasimiana nchini humo. Ripoti pia inasema vurugu la kijinsiya, ikijumuika na vitendo vya mabavu ya kunajisi kihorera babdo yanaendelezwa, kwa utaratibu uliozagaa kila mahali, na wenye kuathirika zaidi na karaha hii ni wanawake na watoto waliopo kwenye kambi za wahamiaji, pamoja na wale wahamaiji wa ndani waliong'olewa makazi kwa sababu ya mapigano. Vile vile ilibainishwa ndani ya ripoti juu ya kuzidi kwa mashambulio dhidi ya wahudumia misaada ya kiutu pamoja na mali zao, hasa katika jimbo la Darfur, hali ambayo, ripoti ilitilia mkazo, huwanyima jamii hiyo uwezo wa kutekeleleza majukumu yao kwa umma muhitaji, kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

   Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeripoti wazalendo 15,000 wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) wamelazimika kuhama makwao na kuelekea Sudan kusini, kwa sababu ya mashambulio ya mara kwa mara yanayofanywa na waasi wa Uganda wa kundi la LRA. Kadhalika, taarifa ya UNHCR imeeleza operesheni zinazoendelezwa karibuni, shirika, na majeshi ya JKK na Rwanda dhidi ya kundi la waasi wa Kinyarwanda waliopo ndani ya Kongo, ni hali iliyochochea raia zaidi kuhajiri nchi. Taarifa iansema wingi wa wahamiaji hawa walitokea mji wa mpakani wa Aba, katika JKK, ambao mnamo mwezi Januari ulihujumiwa mara kadha wa kadha, na kushambuliwa tena hata wiki iliopita. Wahamiaji wa Kongo, waliowasili mji wa Lasu, Sudan kusini waliwaambia wafanyakazi wa UNHCR kwamba mji wao wa Aba, walipokuwa wakiishi watu 100,000 sasa hivi ni mtupu, hauna tena watu. Wakati huo huo, idadi ya raia wa Kongo waliokimbia mashambulio ya waasi wa LRA, katika eneo la kaskazini-magharibi la Dungu, imekiuka wahamiaji 9,000 katika mwezi Januari. Kuhusu eneo la kusini, operesheni za pamoja za majeshi ya JKK na Rwanda dhidi ya waasi wa FDLR, zimelipatia Shirika la UNHCR upenu wa kuweza kuwarejesha wahamiaji 3,000 Rwanda katika wiki za karibuni.

   Choi Young-jin, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Cote d'Ivoire ametoa mwito wa kutaka kuchapishwe, rasmi, ratiba inayosarifika itakayoelezea kihakika malengo na hatua kadha za kuchukuliwa kwenye matayarisho ya uchaguzi wa uraisi utakaofanyika nchini baadaye mwaka huu. Aliyasema haya mapema leo katika mji wa Ougadougou, alipokutana na Kamati ya Utathmini na Usimamizi wa mapatano ya amani kwa Cote d'Ivoire. Alisema raia 4,600,000 wameshapokea vitambulisho, hali ambayo inaashiria hamu kuu ya umma wa Cote d'Ivoire kukomesha mizozo ya kisiasa na kurudisha amani nchini mwao.

   Ofisi ya Mratibu wa Misaada ya Kiutu wa UM kwa Maeneo Yaliokaliwa ya WaFalastina imeripoti skuli tatu zinazotumiwa, kama mastakimu ya muda, kwa watu waliong'olewa makazi, skuli zinazoendeshwa na UNRWA, bado zinahudumia kihali umma muhitaji 360 kwenye Tarafa ya Ghaza. Lakini jumla halisi ya watu walionyimwa makazi haijulikani bado. Halkadhalika, UNRWA imemripoti inasaidia kwenye kampeni ya kuwachanja watoto wa skuli 120,000 dhidi ya shurua na matumbwitumbwi. Operesheni hizi vile vile zinajumlisha mafunzo ya kujikinga na maradhi ya kuambukiza, na kila mwanafunzi anatarajiwa kupatiwa dozi ya Vitamini A. Shirika la UM juu ya Udhibiti wa Idadi ya Watu (UNFPA) limeripoti wasiwasi juu ya kuongezeka kwa vifo vya kwenye uzazi, na uharibifu wa mimba, uliodhihirika kujiri katika Ghaza, kufuatia mashambulio ya karibuni kwenye eneo hilo. Kuhusu chakula, Shirika la Miradi ya Chakula Duniani (WFP) limeripoti mboga mboga hupatikana katika Ghaza, lakini wakazi wa hapo, kwa sababu ya hali dhaifu kiuchumi, hawamudu kamwe nyama wala mayai kutokana na bei ghali ya chakula iliosababishwa na upungufu wa malisho ya wanyama. Ofisi ya OCHA pia imeripoti makumi elfu ya watu wa Ghaza hawana uwezo wa kupata maji ya bomba, na maskuli nayo pia yanashuhudia uhaba mkubwa maji safi ya kunywa!