Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu litazingatia marekibisho ya mfumo wa BU

Baraza Kuu litazingatia marekibisho ya mfumo wa BU

Wiki hii, mnamo tarehe 19 Februari, wawakilishi wa Mataifa Wanachama wa Baraza Kuu watakusanyika kwenye Makao Makuu ya UM kujadiliana juu ya ile rai ya kuleta marekibisho kwenye mfumo wa Baraza la Usalama, kwa lengo la kuhakikisha kazi za taasisi hii ya kimataifa zitawakilisha, kwa usawa, na kwa haki matakwa na mahitaji hakika ya wanachama wote wa UM, yatakayolingana na hali halisi ilivyo kwenye uhusiano wa kimataifa wa karne ya ishirini na moja.

Mwakilishi wa Kudumu wa Afghanistan katika UM, Balozi Zahir Tanin, mwenyekiti wa majadiliano hayo, Ijumaa iliopita alikutana na waandishi habari wa kimataifa katika Makuu Makuu na aliwaeleza kwamba kikao kijacho kitawathibitishia wachongezi, wasiochoka kukejeli kazi za UM, kwamba rai ya kuleta marekibisho, kwenye mfumo wa Baraza la Usalama, si porojo tena au kauli ya ndoto za mabalozi wanaokutana kwenye hafla za michapalo na maakuli. Ajenda ya kuzingatia marekibisho kwenye Baraza la Usalama ilipitishwa na azimio la Baraza Kuu, nambari 62, mshazari 557 (62/557), azimio liliopitishwa kwa kauli moja na wajumbe wote wa kimataifa, mnamo tarehe 15 Septemba 2008. Azimio lilitilia mkazo ya kuwa mashauriano kuhusu mageuzi kwenye Baraza la Usalama yaanzishwe, haraka, kabla mwezi Machi 2009 kumalizika. Tutakupatieni taarifa zaidi juu ya mazungumzo haya mnamo siku za usoni.