Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNEP inahimiza uwekezaji wa mazingira uongezwe kuimarisha uchumi wa dunia

UNEP inahimiza uwekezaji wa mazingira uongezwe kuimarisha uchumi wa dunia

Ripoti iliotolewa Ijumatatu na Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) imebainisha awamu ya tatu ya furushi la mradi wa kuwekeza dola trilioni 2 na nusu, zinazohitajika kufufua uchumi wa dunia unaofungamana na mazingira bora, yalio safi na salama.

Ripoti hii iliwasilishwa mjini Nairobi wakati wa ufunguzi wa majadiliano ya mkutano wa kimataifa, wa kiwango cha mawaziri, unaofanyika wiki hii Kenya. Iliashiriwa kwenye ripoti kwamba pindi dola bilioni 750 zitawekezwa kwenye huduma za kimazingira, kuna uwezekano mkubwa wa kufufua uchumi wa kimataifa kwa kasi zaidi, kutoka ule mzoroto ulioselelea hivi sasa duniani. Miradi hii inaashiriwa itakapotekelezwa, itasaidia kuchochea uvumbuzi wa teknolojia mpya ya kuhifadhi mazingira, ilio safi, yenye uwezo wa kurudisha utulivu na kufufua ajira ya vibarua vinavyohishimika. Wakati huo huo, kadhia hizo zitaziwezesha nchi husika kupunguza tegemeo lao la nishati za kaboni, pamoja na kupunguza umwagaji wa hewa chafu angani. Nakala ya ripoti, yenye kichwa cha maneno kinachosema ‘Makubaliano Mapya ya Mazingira Imara Duniani', ilikabidhiwa mawaziri wa mazingira zaidi ya 100, waliohudhuria kikao cha Nairobi, kama kiuasumu dhidi ya mizozo ya kiuchumi iliokabili ulimwengu wa sasa. Achim Steiner, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira alisema kwenye risala yake kwamba ukuaji wa haraka wa uchumi wa dunia unategemea zaidi uekezaji kwenye ile miradi ya kuimarisha mazingira. Alitoa mfano wa baadhi ya mataifa yenye uchumi mkuu, yalioamua kujihusisha na mwelekeo huo katika kufufua uchumi wao, alisema, kwa mfano Jamhuri ya Korea (Korea ya Kusini), pamoja na Marekani na Uchina ni mataifa yalioamua kuweka kando mabilioni ya fedha za kutumiwa kwenye miradi ya kimazingira itakayosaidia kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yao.