Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC kuhusu juhudi za UM za kukomesha uhalifu wa mipangilio

UNODC kuhusu juhudi za UM za kukomesha uhalifu wa mipangilio

Wiki hii tutaendelea na taarifa zetu kuhusu juhudi za UM katika kukomesha uhalifu wa mipangilio, ambao huhatarisha usalama na amani ya umma wa kimataifa.

Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) Alkhamisi iliwakilisha, mbele ya waandishi habari waliopo Makao Makuu, taarifa yenye mada isemayo ‘Ripoti ya Kimataifa juu ya Biashara ya Magendo ya Kuchuuza Wanadamu'.  Kwa mujibu wa ripoti, ambayo kwa mara ya kwanza inawakilisha kadirio la janga hili kimataifa kuhusu biashara ya kuchuuza wanadamu, ilibainisha utaratibu unaotumiwa kutorosha wanadamu wanaoshurutishwa kushiriki kwenye vibarua vya lazima, hufungamana zaidi na uhalifu wa kudhalilisha wanawake na watoto wa kike.  Jambo liliowashtua zaidi watafiti wa Ofisi ya UNODC walipokuwa wanachanganua takwimu zao ni pale walipogundua ya kuwa, fungu kubwa la watu wanao'ongoza biashara hii haramu, katika asilimia 30 ya mataifa yalioupatia UM takwimu za wahusika wa kijinsia, walikuwa ni wanawake. Watu wanaoshirikishwa kwenye vibarua vya kulazimishwa hujumlisha asilimia 18 ya umma unaotoroshwa makwao na wahalifu wa mipangilio. Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya UNODC, Antonio Maria Costa amezihimiza serikali za wanachama wa UM kufanya kila wawezalo, kutekeleza kikamilifu, zile sheria zinazoambatana na Mkataba wa UM dhidi ya Biashara ya Kuchuuza Wanadamu kwa Ajira ya Kulazimishwa, chombo ambacho kilifanywa sheria ya kimataifa katika 2003. Vile vile Costa alihamasisha serikali na wataalamu wa ilimu za kijamii, kote ulimwenguni, kujumuisha mifumo ya kisasa pale wanapokusanya taarifa za uchunguzi wao, zinazohitajika kuchanganua udhibiti bora wa tatizo hili la magendo ya kuchuuza wanadamu kimataifa.

Baadaye alasiri, kadhalika, kwenye Makao Makuu kulifanyika tafrija maalumu na Ofisi ya UM juu ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya na Uhalifu (UNODC) ambapo Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Antonio Maria Costa, alimtunukia rasmi Mira Sorvino, mwiigizaji maarufu wa Kimarekani, wa michezo ya sinema wadhifa wa kuwa Balozi Mfadhili atakayehusika katika zile jitihadi za kimataifa, za kukomesha biashara haramu ya kuchuuza wanadamu, wanaotoroshwa makwao na kutumiwa kwenye vibarua vya lazima, nje ya sheria. Vitendo hivi haramu hufananishwa na wanasheria wa kanuni za kimataifa sawa na utumwa mamboleo. Hali kadhalika, tarehe iliofanyiwa tafrija za Ofisi ya UNODC, yaani tarehe 12 Februari (2009) inaadhimisha miaka 200 ya kuzaliwa kwa Abraham Lincoln, aliyekuwa Raisi wa Marekani, aliyeongoza ukombozi wa watumwa nchini mwao. Sorvino alisisitiza kwenye risala alioitoa kwenye taadhima za kuteuliwa Balozi Mfadhili wa Ofisi ya UNODC, kwamba ni muhimu kwa umma wa kimataifa kutambua kama biashara ya kuchuuza watu wanaotoroshwa makwao haitofautiani na utumwa mamboleo. Utambuzi huu, alitilia mkazo, ni hatua ambayo anaamini husaidia katika "kurekibisha mawazo ya umma wa kimataifa dhidi ya mateso wanayopata waathirika wa ulimwengu wa karaha ya utumwa mamboleo" na, hatimaye, anatumai itasaidia pia kulikomesha janga hili karaha milele.