Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na pale

Hapa na pale

KM Ban Ki-moon ameripotiwa kushtushwa, kwa shambulio la kujitoa mhanga dhidi ya wachaMngu wa KiShia, liliotukia Ijumaa karibu na Baghdad. Kadhalika, KM alisema ameshtushwa na mashambulio mengine kama hayo yaliotukia majuzi Iraq ambayo yalisababisha darzeni za vifo na kujeruhi raia kadha wa kadha, ikijumlisha fungu kubwa la watoto wadogo na wanawake. KM alisisitiza hakuna sera ulimwenguni inayohalalisha vitendo hivi, si ya kidini wala kisiasa, na alikumbusha walimwengu wanawajibika, pote walipo, kulaani kwa lugha nzito kabisa makosa kama haya ya jinai kuu dhidi ya wanadamu. KM aliusihi umma wa Iraq kupinga kabisa jaribio katili linalotaka kuchochea fujo za kiitikadi nchini mwao, na aliwataka viongozi wa Iraq kuungana pamoja, kwa moyo wa kuhishimiana na uelewano wa kizalendo, kama walivyofanya wakati walipokwenda kupiga kura karibuni kwenye uchaguzi wa majimbo, uchaguzi ambao ulifanyika mwezi uliopita bila fujo.

Hapa na pale

Alkhamisi usiku KM alitangaza kuwa ameteua wawakilishi wa Bodi la Uchunguzi la UM litakalojaribu kuchanganua matukio ya karibuni Ghaza, tume ambayo ilishaanzisha shughuli zake mjini New York, na inatazamiwa kueleka kwenye eneo husika katika siku za karibuni. Bodi la Uchunguzi juu ya Ghaza linaoongozwa na Ian Martin wa kutoka Uingereza, Larry Johnson (Marekani), Sinha Basnayake (Sri Lanka) na Liuteni Kanali Patrick Eichenberger wa Uswiss. Madhumuni ya KM kuunda Bodi hili la Uchunguzi ni kufanya mapitio, na kuchunguza rasmi vitendo viliovyokiuka sheria ya kiutu vilivyotukia kwenye Tarafa ya Ghaza baina ya tarehe 27 Disemba 2008 mpaka 19 Januari 2009, matukio ambayo yalizusha vifo na majeruhi kadha ya raia, na pia kusababisha uharibufi mkubwa wa majengo ya UM, na hata kuathiri operesheni zake za kuhudumia kihali umma. Baada ya kukamilisha uchunguzi wao, wawakilishi wa Bodi la Uchunguzi wataripoti matukio yao, moja kwa moja kwa KM, ambaye ataipitia ripoti hiyo na kuamua ni hatua za aina gani zichukuliwe na UM wakati huo kuhusu matukio ya Ghaza.

   Wataalamu wajuzi wa kusafisha mabomu yaliotegwa ardhini, kutoka ile Taasisi ya UM Inayohudumia Ufyekaji wa Mabomu Yaliotegwa (MAS) wameripoti kushuhudia katika Mji wa Ghaza mabomu makubwa yanayotumiwa na ndege za kijeshi pamoja na makombora ya kutupia silaha haribifu za fosforasi zenye kuunguza watu na vitu, kwa urahisi zilizokusanywa kwenye sehemu za eneo hilo. Walisema hawakufanikiwa bado kutathminia kiwango cha uharibifu uliofanywa na silaha hizo katika Ghaza kufuatia mapigano yaliopamba huko wiki chache zilizopita. Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) imeripoti timu ya mabingwa hawa wa UM inaendelea kukusanya silaha zilizoshindwa kuripuka wakati wa mashambulizi ya Mji wa Ghaza, lakini imehadharisha ya kuwa kwa sababu ya vikwazo visioruhusu zana na vifaa vinavyohitajika kuendeleza kazi zao kuingizwa Ghaza wataalamu wa UM hawatoweza kuangamiza zile silaha haribifu na maututi zilizoenea kwenye eneo.

   Wakati huo huo, Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) linakadiria nyumba 14,000 ziada katika Tarafa ya Ghaza, ama ziliharibiwa kwa sehemu au kikamilifu wakati wa mapigano. Katika juhudi za kukidhi mahitaji ya makazi ya muda mrefu kwa wale walion'golewa makazi, UNDP imaripoti kuwa itazipatia aila /koo 10,000 msaada wa fedha taslimu, wa baina ya dola 1,000 - 3,000, kwa kulingana na ukubwa wa ayali ilivyo, pamoja na hadhi ya kiuchumi na jamii pamoja na kiwango cha uharibifu wa majengo yao. OCHA nayo pia imeripoti wale wafanyakazi wanaohudumia misaada ya kiutu, bado wanaendelea kukabili matatizo ya kunyimwa vibali vya kuingia Ghaza, kwa kupitia kivuko cha Erez. Mathalan, katika mwezi wa Januari watumishi 18 tu wa huduma za kiutu walioruhusiwa na Israel kuingia Ghaza kati ya maombi ya watumishi 178.

   Matokeo mapya ya uchunguzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu janga la kipindupindu katika Zimbabwe yanaonyesha maradhi bado hayajadhibitiwa kama inavyotakiwa, na takwimu zilizosajiliwa kwa sasa zimethibitisha watu 73,000 waliambukizwa na kipindupindu nchini humo, maradhi yaliosababisha vifo 3,524. Vile vile WHO imeripoti vituo vipya vya tiba ya kipindupindu vinaendelea kufunguliwa, na kuongezeka katika sehemu mbalimbali za nchi. Hata hivyo, inakhofiwa kwamba mvua zinazotarajiwa kuwasili karibuni zitazorotisha huduma za afya kwenye baadhi ya majimbo yenye kuhitajia msaada huo. Vile vile jamii inayohudmia misaada ya kiutu inakabiliwa na matatizo ziada ya kudhibiti kipindupindu, yanayotokana na ukosefu wa chakula pamoja na miunndombinu dhaifu ya usafiri, ikichanganyika na mishahara midogo wanayolipwa wahudumia afya Zimbabwe. Kwa mujibu wa ripoti ya WHO, Kampeni ya Ombi la 2009 la kuchangisha msaada wa fedha za kudhibiti kipindupindu Zimbabwe imeweza kupokea asilimia 21 tu ya ombi hilo.