Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna wa Haki za Binadamu aisihi Zimbabwe kufufua utaratibu wa kuhishimu sheria

Kamishna wa Haki za Binadamu aisihi Zimbabwe kufufua utaratibu wa kuhishimu sheria

Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu, Navi Pillay, ametoa mwito maalumu uliopendekeza kwa Serikali mpya ya Muungano wa Taifa katika Zimbabwe, kuchukua hatua za dharura kufufua taratibu za kuhakikisha sheria za nchi zinafuatwa na kuhishimiwa na kila raia.

Kamishna Pillay aliitaka Serikali iyashughulikie yale masuala yenye kuhusu matumizi mabaya ya madaraka kwenye utekelezaji wa sheria, yalioshuhudiwa kujiri siku za nyuma, kufuatia uchaguzi wa taifa kutokana na mvutano wa kisiasa. Alisema mzozo huo ulipalilia tabia karaha ya kupuuza kanuni za nchi, miongoni mwa wenye madaraka, hali ambayo ilizusha ukiukaji mkubwa wa haki za kiutu dhidi ya raia - mathalan, maofisa kadha wa upinzani walipotea, wapinzani wengineo waliteswa na kulazimishwa kukiri, kwa udanganyifu, makosa na wenye madaraka walikutikana hata kuingilia kati uhuru wa mahakama katika kuendeleza shughuli zake. Taarifa ya Kamishna Mkuu wa UM juu ya Haki za Binadamu imeihimiza Serikali mpya ya Zimbabwe kutekeleza majukumu yake yote chini ya sheria ya kimataifa, ikijumlisha upigaji marufuku wa vitendo vyote vya kutesa watu na kuhakikisha uhuru wa mahakama unahishimiwa.