Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ijumanne Baraza la Usalama lilikutana kwenye kikao cha mashauriano ya awali kuzingatia ajenda ya mwezi Februari, kikao kinachoongozwa na Ujapani, taifa linaloshika madaraka ya uraisi wa Baraza kwa mwezi huu. Kadhalika, Baraza la Usalama lilizingatia ripoti kuhusu hali katika Darfur iliowakilishwa na Edmond Mulet, KM Mdogo Msaidizi kwenye Idara ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM.

Ofisi ya Mratibu Maalumu wa UM juu ya Mpango wa Amani katika Mashariki ya Kati (UNSCO) pamoja na Ofisi ya UM juu ya Misaada ya Dharura (OCHA) zimeripoti idadi ya malori yenye kubeba bidhaa na misaada ya kiutu inayoruhusiwa, kila siku, na wenye madaraka Israel kuingia kwenye eneo liliokaliwa la Tarafa ya Ghaza, ni ndogo sana na hairidhishi kukimu mahitaji ya maisha kwa umma. Zaidi ya hilo, orodha ya vitu vilivyoruhusiwa kuingia Ghaza, kwa kupitia vivuko vya mpakani baina ya Israel na Ghaza, ni orodha iliojaa masharti na vizuizi aina kwa aina! Kwa mfano, Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA), Ijumaa iliopitia halikuruhusiwa kuingiza Ghaza mifuko ya plastiki inayotumiwa kugawia vifurushi vya chakula kila siku kwa watu 20,000 wa eneo husika.

Wakati huo huo, skuli tatu zisiokuwa za UNRWA, ndio bado hutumiwa kama mamstakimu ya muda kwa wakazi 40,000 walion’golewa mastakimu.

Shirika la Afya Duniani (WHO) pia limeripoti wingi wa vituo vyao vya afya katika Ghaza sasa vinajitahidi kuendeleza shughuli zao kwa utaratibu wa kawaida, baada ya kufadhiliwa madawa na vifaa vya kuhudumia afya kwa wingi. Licha ya hayo, UNRWA imeripoti, bado kuna upungufu mkubwa wa madawa ya kutibu maradhi ya kiakili, tiba ambayo inahitajika haraka, hususan kwa wale raia walioghumiwa na mishtuko ya mashambulio ya vikosi vya uvamizi, hali iliowaathiri kiakili. Kadhalika iliripotiwa kuna upungufu sindano, mashine za kupumilia na vifaa vya kufuatilia hali ya kutokuwa na hisia wakati wa matibabu.

UNRWA imeripoti kuwa itahitajia iruhusiwe kuingiza Ghaza, haraka iwezekanavyo, vifaa vinavyohitajika kuhudumia umma kimaisha, ikijumlisha mablangeti, magodoro, maturubali ya kuezekea makazi ya muda, vifaa vya kupikia na matumizi ya jikoni pamoja na zana za kudhibiti usafi wa mazingira, matangi ya maji, nguo na vile vile mahema.

Ofisi ya UNSCO pia imeripoti wakazi wa Tarafa ya Ghaza bado wanaendelea kukatiwa umeme, na kuna sehemu za eneo hilo ambazo umeme hukatwa kwa muda wa saa 12 kila siku.

KM Ban Ki-moon amemtumia raisi wa Baraza la Usalama barua yenye kuelezea masikitiko yake juu ya kupwelewa Mataifa Wanachama katika kuchangisha vikosi ziada vinavyohitajika kuhudumia Shirika la Ulinzi Amani katika JKK la MONUC. Alisema kwenye barua yake kwamba baada ya kuomba msaada huo kutoka nchi 49 zilizochangisha vikosi vyao kwenye huduma za amani za UM, pamoja na kutoka nchi 12 nyengine zilizopendekeza kufanya hivyo amefanikiwa kupokea ahadi ya Bangladesh kuwa itachangisha batalioni moja ya vikosi vya miguu, kombania moja ya wahandisi wa kijeshi na kikundi kimoja cha polisi. Kadhalika KM alisema Ubelgiji imekubali kuipatia MONUC ndege ya kijeshi ya aina ya C-130, na Mataifa Wanachama matano mengine pia yameahidi kupeleka timu ya wataalamu wanaohusika na kadhia ya upelelezi dhidi ya maadui.