Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KM afanya ziara ya dharura Afghanistan

KM afanya ziara ya dharura Afghanistan

Ijumatano KM Ban Ki-moon alifanya ziara ya ghafla katika Afghanistan. Alipokuwepo huko, KM aliahidi UM utaendelea kuchangia, kwa kila njia, kwenye zile huduma za maendeleo zinazotakikana, kidharura, kuimarisha usalama na amani ya taifa.

Baada ya kutumia saa chache katika Afghanistan KM alielekea Pakistan na aliwasili Islamabad kwa ziara rasmi, ya kwanza, nchini humo. Alipokuwepo Islamabad alikuwa na mazungumzo na maofisa kadha wa Serikali, na pia alikutana na watumishi wa UM waliopo Pakistan. Alikutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu, Yosaf Raza Gillani ambapo KM aliisihi Serikali juu ya umuhimu wa kurudisha uhusiano wa kirafiki baina ya Pakistan na taifa jirani la Bara Hindi. Kuhusu mauaji ya 2007 ya Benazir Bhutto, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, KM alibainisha kuwa mnamo siku za karibuni ataanzisha Kamisheni ya Uchunguzi huru kuhusu tukio hilo. Vile vile KM alikutana na Raisi wa Pakistan Asif Ali Zardari kwa mashauriano. Kabla ya hapo KM alishuhudia utiaji sahihi wa “Warka wa Kuunganisha Miradi ya UM juu ya Maendeleo Pakistan”, mapatano yaliotiwa sahihi na wawakilishi wa Serikali ya Pakistan pamoja na Timu ya Watumishi Wakazi wa UM waliopo nchini. Kufuatia shughuli hizo, KM alionana na waandishi habari, na kwenye risala yake alisisitiza ya kuwa UM unaunga mkono juhudi zote za Serikali ya Pakistan za kupiga vita vitisho vya ugaidi, na pia zile nidhamu za kulisaidia taifa kujikomboa kutoka mizozo ya fedha na ile ya kiuchumi.