Hapa na Pale
Vuguvugu la kisiasa, liliotanda Bukini kwa sasa, linamtia wasiwasi KM Ban Ki-moon kuhusu utulivu na amani ya taifa. Kufuatia ombi la Serikali ya Bukini, KM ameamua kumpeleka Haile Menkerios, aliye KM Msaidizi kwa Masuala ya Kisiasa kusailia hali Bukini, ambaye anatarajiwa kutathminia mchango wa UM unaohitajika kusaidia kuzuia vurugu lisisambae zaidi kitaifa na, hatimaye, kurudisha amani na utulivu nchini Bukini. Menkerios atakuwepo Bukini kuanzia tarehe 07 mpaka 10 Februari, na atakutana kwa mazungumzo na ushauri pamoja na maofisa wa Serikali na wawakilishi wa makundi yote yaliofungamana na mzozo uliofumka majuzi nchini humo.
Mjumbe Maalumu wa KM kwa Watoto kwenye Hali ya Mizozo, Radhika Coomaraswamy, amekamilisha ziara ya siku nne kwenye maeneo yaliokaliwa kimabavu ya WaFalastina na katika Israel kusini. Alipokuwepo kwenye eneo alifanya ukaguzi kuhusu athari za afya ya akili kwa watoto, zinazoambatana na mazingira ya uhasama. Alinakiliwa akisema ya kuwa licha ya mapigano kusimamishwa kitambo katika Tarafa ya Ghaza, watoto bado wanaendelea kuteseka, na wameonekana kughumiwa sana kiakili na ile hisia iliojaa wasiwasi kwamba hali ya eneo lao haina salama.
Mjumbe Maalumu wa KM kwa Sudan, Ashraf Jehangir Khan, Alkhamisi alihutubia Baraza la Usalama na alielezea matokeo ya ripoti mpya juu ya hali nchini Sudan. Alisisitiza kwenye taarifa yake kwamba Mapatano ya Amani ya Jumla yaliofikiwa na makundi yaliohusika na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoshtadi nchini kwa muda mrefu, ndio pekee yenye kujumuisha msingi muhimu wenye matumaini ya kurudisha utulivu na amani Sudan Kaskazini na Kusini. Alihadharisha ya kuwa umma wa Sudan ndio utakaohukumu baadaye kama majukumu ya kurudisha amani nchini mwao yanatekelezwa, kama inavyostahiki, na viongozi, makundi husika, na jamii ya kimataifa, halkadhalika.
Rodolphe Adada, Mpatanishi Maalumu Bia wa UM-UA kwa Darfur amekamilisha ziara ya siku mbili Chad, ambapo alikutana na Khalil Ibrahim, kiongozi wa kundi la waasi la Sudan la JEM ambaye alimwarifu kuwa atahamisha wapiganaji wake kutoka eneo la uhasama wa karibuni katika Muhajeriya, baada ya vikosi vya amani kwa Darfur vya UM-UA, yaani vikosi vya UNAMID, vilipoahidi kusalia kwenye eneo kwa makusudio ya kuimarisha ulinzi wa raia, kufuatia ombi la KM la kuwapatia wakazi wa Muhajeriya usalama dhidi ya mapigano. Adada amechukua hatua ya kushauriana na makundi yote yanayoambatana na mgogoro wa Darfur kwa madhumuni ya kujenga uhusiano mzuri wa kikazi, hususan baada ya mifumko ya vurugu majuzi katika Muhajeriya. UNAMID imethibitisha wafuasi wa JEM wameshaondoshwa Muhajeriya na hali huko inasemekana ni shwari Alkhamisi, licha ya kuwa bado kuna wasiwasi. Wahamiaji wa ndani 3,000 pia wamesalia kwenye eneo la karibu na kambi za UNAMID kutafuta hifadhi. UNAMID imeripoti kuwa itaendelea kufuatilia hali ya usalama kwenye eneo. Wakati huo huo vikosi vya UNAMID vinashiriki kuhudumia jamii inayohusijka na misaada ya kiutu kwenye ujenzi wa mastakimu ya muda kwa raia waliong’olewa makazi. Hivi sasa mahema 17 yameshaezekwa katika sehemu ya Wadi, iliopo Magharibi ya kambi ya Zam Zam.
Naibu KM juu ya Masuala ya Kiutu na Misaada ya Dharura, John Holmes ameripotiwa kuelekea Kinshasa, katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) ambapo atawasili Ijumaa kwa ziara ya siku nne, ili kutathminia mahitaji ya dharura ya kiutu kwa umma ulioathirika na vurugu na fujo za wiki za karibuni kwenye eneo la mashariki. UM unasisitiza fujo lazima zikomeshwe, halan, kieneo. Vile vile Holmes anatazamiwa atapendekeza vitendo vyote vya kutumia mabavu dhidi ya raia, hususan mateso na udhalilishaji wa kijinsia, navyo pia vikomeshwe haraka. Holmes atatembelea sehemu kadha za nchi, na atakutana na wenye madaraka wa kienyeji na maofisa wa kiserikali, pamoja na kukutana na wahamiaji waliong’olewa makazi na aila zilizosaidia kuwapatia makazi ya muda, na wahusika wa misaada ya kihali. Holmes atakamilisha ziara yake katika JKK Februari 10, 2009.
Ijumatano, Shirika la UM juu ya Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) limeripoti kwamba lilifanikiwa kuwakomboa watoto wapiganaji 28 kutoka majeshi ya mgambo. Hii ndio shuruti mojawapo itakayowezesha wafuasi wa majeshi ya mgambo kuunganishwa na jeshi la taifa baada ya kuruhusu kuwachiwa huru watoto chini ya umri wa miaka 18. Jumla ya watoto waliokombolewa, wiki iliopita pekee, na MONUC kutoka wanamgambo sasa imefikia 220. Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) linawahudumia kihali, sasa hivi, watoto hawo na kuwatayarisha kurejea kwenye maisha ya kikawaida ya kiraia.