Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Alain Le Roy, Naibu KM juu ya Operesheni za Ulinzi Amani ameripotiwa akiendelea na ziara ya kutembelea Afghanistan, ambapo alipokutana na waandishi habari alisema UM utaendelea kuongoza shughuli zake nchini humo, na utahakikisha uchaguzi utafanyika kwa wakati, kwa uwazi na kwa haki. Alisema UM utabakia kwa muda mrefu Afghanistan, kuimarisha maendeleo yaliopatikana kutokana na mchango wa wazalendo wenyewe, hususan katika kukuza afya bora, kuimarisha ilimu, na kusimamia shughuli za kufyeka mabomu yaliotegwa, huduma ambazo UM utasaidia kuzihimilia na kuziendeleza Afghanistan kwa siku zijazo.

John Holmes, Naibu KM kwa Masuala ya Kiutu na Mshauri wa Misaada ya Dharura anaendelea na safari ya kuzuru JKK. Ijumatatu alizuru miji ya Dungun na Doruma katika jimbo la Haut Uele, eneo ambalo hushambuliwa mara kwa mara na waasi wa Uganda wa kundi la LRA. Waasi hawa kawaida huhujumu raia na kuwaua kihorera, na hutumia ukatili uliokiuka mipaka. Kwa mujibu wa UM mashambulio ya waasi wa LRA yalisababisha vifo kwa mamia ya raia, na waasi pia waliwatorosha mamia ya watoto wadogo ambao baadaye huwashurutisha kushiriki kwenye mapigano haramu. Holmes alikutana na waathirika wa mashambulio maututi ya LRA, na alitathminia taratibu za kuchukuliwa na vikosi vya kimataifa kuimarisha zaidi hifadhi ya raia husika. Holmes alilaani ukatili wa LRA, na alivihimiza vikosi vya Shirika la Ulinzi Amani katika JKK (MONUC) kuipa umuhimu wa hali ya juu suala la kuwahifadhi raia katika eneo zima la Kongo mashariki. Baada ya hapo Holmes alielekea Kinshasa, ambapo atakutana na maofisa wa serikali, mabalozi wanaowakilisha nchi za kigeni katika JKK pamoja na watumishi wakazi wa UM. Holmes atakamilisha ziara yake katika JKK Ijumanne.

Shirika la UM juu ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limearifu ya kuwa linatayarisha kuanzisha kitabu cha ramani ya zile lugha za kimataifa zenye hatari ya kuangamia au kutoweka. Tukio hilo litafanyika wiki ijayo kwenye mji wa Paris, Ufaransa. Ramani itachapishwa kwa mara ya kwanza na UNESCO kuwa ni chombo cha mtandao wenye kutumia utaratibu wa kubadilishana taarifa juu ya lugha husika karibu 2,500. Huduma hii itafadhiliwa bure na UNESCO kote ulimwenguni kwa wale watu wenye kutafuta taarifa hizo za lugha adimu.

Kamati Ndogo ya Kisayansi na Ufundi ya Kamati ya UM juu ya Matumizi ya Amani ya Anga Ijumatatu imeanza mijadala ya kikao cha 46 mjini Vienna, Austria kuzingatia hatari ya vyombo vinavyoruka karibu na Ardhi, na pia kusailia mfumo salama wa kudhibiti vyanzo vya nishati ya kinyuklia angani, pamoja na kujadilia taratibu za kupunguza takataka za kwenye anga nje ya dunia. Majadiliano haya yanatarajiwa kuendelea hadi tarehe 20 Februari (2009).