Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Mpatanishi Mkuu wa Pamoja wa UM-UA kwa Darfur, Djibril Yipéné Bassolé ametoa taarifa ya kupongeza Seikali ya Sudan pamoja na kundi la waasi la JEM, kwa kuridhia kukutana Doha, Qatar kwa mazungumzo ya kusimamisha uhasama yaliofanyika Ijumanne asubuhi. Bassolé alisisitiza juu ya umuhimu wa kuwajumuisha wadau wote wanaohusika na suala la Darfur, kwenye majadiliano ya kuimarisha amani. Hii ni mara ya kwanza kwa makundi haya mawili yanayohasimiana Sudan kukubali kukutana uso kwa uso, tangu 2007 baada ya mkutano wa upatanishi uliofanyika kwenye mji wa Abuja, Nigeria.

Shirika la MONUC limeripoti wapiganaji wenye asili ya KiHutu 150 na aila zao, waliotokea Rwanda, wametoweka kwenye kambi ya mji wa Kasiki, iliopo kilomita 200 kaskazini ya Goma baada ya kuahidi kutaka kurejeshwa makwao, kwa hiyari, na UM katika tarehe 08 Februari (2009) baada ya kupokonywa silaha na MONUC mwzei Julai 2008. Wapiganaji hawa walihusika na kundi la FDLR. Wanajeshi wa MONUC wanaendelea kuwatafuta wapiganaji hawo ili kuwarudisha Rwanda kama walivyopanga hapo kabla.

Shirika la UM Linalofarajia Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA) wiki iliopita liliweza kugawa vitabu vya kuandikia, kwa skuli kumi na moja kwenye eneo la Beit Hanoun, Ghaza. Hata hivyo, UNRWA imeripoti kulazimika kusimamisha ugawaji ziada wa vifaa vya skuli katika eneo hilo, kwa sababu ya kunyimwa ruhusa ya kuagiza vitabu vya kuandikiia. Ripoti ilisema UNRWA bado wanasubiri kibali cha kuagizishia karatasi za kutumiwa kuchapishia vitabu ziada kwa skuli za Ghaza, hali ambayo inawanyima asilimia 60 ya watoto vifaa vya masomo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria baina ya watu 25,000 mpaka 50,000 wanaoishi kwenye Tarafa ya Ghaza watahitajia kupatiwa, haraka, tiba ya muda mrefu ya maradhi ya akili, kwa sababu ya athari mbaya zilizotokana na mashambulizi ya karibuni kwenye eneo lao.

Wakati walimwengu wanaadhimisha kubuniwa kwa serikali ya muungano wa taifa Zimbabwe, na kuapishwa kwa Waziri Mkuu mpya, Shirika la UM juu ya Mfuko wa Maendeleo kwa Watoto (UNICEF) limeripoti Ijumanne asilimia 94 za skuli vijijini Zimbabwe bado zimefungwa. UNESCO imehimiza serikali mpya kulipa suala la kufungua skuli umuhimu wa hali ya juu, pamoja na huduma za kuimarisha sekta ya ilimu kitaifa.

Shirika la UM juu ya Upatanishi wa Amani ya Kusini na Kaskazini (UNMIS) limeanzisha rasmi kwenye eneo la Ed Damazin, katika Jimbo la Blue Nile, ule Mpango wa Kupokonya Silaha Wapiganaji wa Majeshi ya Mgambo. Taadhima hiyo ilihudhuriwa na maofisa wa ngazi za juu wa serikali, pamoja na wawakilishi wa nchi wahisani na wajumbe waliowakilisha UM. Mpango huo, unaojulikana kwa umaarufu kama Mpango wa DDR, unalenga kupokonya silaha wapiganaji 5,000 katika Jimbo la Blue Nile, kati ya jumla ya wapiganaji 180,000.

Michel Sidibé, Mkurugenzi Mkuu mpya wa Jumuiya ya Mashirika ya UM Dhidi ya UKIMWI (UNAIDS) amenakiliwa akisema atayapa umuhimu, wa kiwango cha juu, yale masuala yanayohusu uwezo wa mtu kupata huduma kinga dhidi ya virusi vya UKIMWI, na katika kuwapatia tiba, uangalizi bora na misaada inayofaa kudhibiti maradhi. Sidibé aliyasema hayo alipokuwa akizuru kitongoji cha Khayelitsha, Afrika Kuisni, kwenye ziara yake ya awali nchini humo. Aliitaka jumuiya ya kimataifa kutoruhusu mizozo ya kiuchumi iliopamba ulimwenguni kwa sasa kuzorotisha juhudi za kukamilisha ahadi ya kuupatia umma kinga dhidi ya VVU. Kwa mujibu wa takwimu za Jumuiya ya UNAIDS, inakadiriwa katika 2010 kutahitajika mchango wa dola bilioni 25 kuhudumia miradi ya kudhibiti UKIMWI katika nchi maskini na katika zile nchi zenye mapato ya wastani, jumla ambayo imekiuka kwa dola milioni 11 ya jumla ya fedha ziliopo sasa kuhudumia kadhia hiyo ya afya.