Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kumbukumbu za majadiliano kuzingatia muongezeko wa vurugu katika Ghaza

Kumbukumbu za majadiliano kuzingatia muongezeko wa vurugu katika Ghaza

Ifuatayo ni kumbukumbu ya kikao cha Baraza la Usalama, kilichofanyika Ijumatano kwenye Makao Makuu ya UM, kuanzia saa 12:40 magharibi hadi saa 2:45 usiku.~

Kwenye risala aliowasilisha KM Ban Ki-moon mbele ya kikao hicho, alikumbusha ya kwamba mtiririko wa mgogoro uliofumka karibuni umeathiri raia wa KiFalastina, wanaojumuisha mfumo wa jamii hakika ya Tarafa ya Ghaza, na kuathiri mpango wa amani katik Mashariki ya Kati pamoja na utulivu wa eneo na amani ya ulimwengu, kutokana na hali ya washirika wanaoonyesha kutojali, kwa kuambatana na mashambulio yasiobagua ya makombora ya WaFalastina walio wafuasi wa kundi la Hamas [dhidi ya Israel], na kutokana na vitendo vya kutumia mabavu yasiowiana, vilivyodhihirishwa na hujuma na mashambulio yanayoongozwa na majeshi ya Israel dhidi ya wakazi wa Ghaza. KM alihadharisha hali hii ikiselelea itahatarisha amani ya eneo zima la Mashariki ya Kati na mgogoro huenda ukakiuka kiwango cha vurugu liliojaa mauaji na maangamizi.” Aliendelea kueleza vurugu na matumizi ya nguvu katika Ghaza yamezusha hali ya kutisha sana kwa WaFalastina milioni 1.5 wanaoishi kwenye mazingira yaliopambwa na mashambulio mazito ya mabomu. Alishtumu na kulaani vikali, kwa msiamamo ulio wazi “mashambulizi ya makombora ya Kundi la Hamas na wapambanaji wengine wa KiFalastina” dhidi ya Israel. Vile vile KM alisisitiza kuwa anashutumu “mashambulio yaliopita kiasi ya vikosi vya Israel” katika Ghaza. Aliyataka makundi yote husika na uhasama huo, kuhishimu na kutekeleza sheria za kiutu za kimataifa”, kwa kuhakikisha wanawapatia raia hifadhi, maana hili ndio funga la umma unaoathirika zaidi na mapigano. Halkadhalika, KM alikumbusha kwamba tusisahau, licha ya kuwa mapigano yamepamba, kiini halisi cha mzozo huo ni lile suala la ukaliaji kimabavu wa maeneo ya WaFalastina, ukaliaji ambao ni lazima usitishwe ili, hatimaye, uhakikishe kunazaliwa Taifa Huru la Falastina, litakaloishi jirani na Israel kwa usalama na amani.

Riyad Mansour, Mwangalizi wa Kudumu wa Falastina katika UM yeye alifananisha mashambulio ya Israel Ijumatano kuwa ni ya “uchokozi uliokamilisha siku ya tano mfululizo, dhidi ya umma wa Ghaza, mashambulio yaliokwisha kuua zaidi ya watu 380 na kujeruhi watu 1,800 ziada, ikijumlisha wanawake na watoto wasio hatia.

Gabriela Shalev, Balozi wa Israel katika UM, alisistiza taifa lake limelazimika Ijumamosi kuanzisha operesheni za kijeshi katika Tarafa ya Ghaza, kwa lengo la kuwapatia raia zake hifadhi na ulinzi dhidi ya alichokiita “mfululizo wa makombora” yanayomiminikia kutoka eneo hilo la WaFalastina.

Giadalla A. Talhi, Mjumbe wa Kudumu wa Libya katika UM alikumbusha kwenye risala yake kwamba maafikiano ya kusimamisha mapigano baina ya WaFalastina na Waisraili, yaliokamilishwa mwezi Juni 2008, chini ya uongozi wa Misri, yalieleza ya kuwa miongoni mwa ahadi zilizoafikiwa ni kwamba Israel itafungua mipaka na kuruhusu vitu kuingizwa Ghaza kukidhi mahitaji ya umma kimaisha. Wakati WaFalastina, kwa upande wao, walihishimu “kama ibada” masharti ya maafikiano hayo, Balozi wa Libya aliendelea kusema, hata hivyo, WaIsraili waliamua kuharamisha mapatano yao mara 190, na kusababisha vifo vya raia 25 wa KiFalastina, na wakati huo huo kutofungua, kwa mfululizo, vituo vya mipaka vinavyotumiwa kuingiza bidhaa za kukidhi mahitaji ya wakazi wa Ghaza. Mnamo Novemba 04, 2008, alieendelea kueleza Balozi wa Libya, majeshi ya Israel yaliingia eneo la mashariki katika Ghaza, bila ya kuchokozwa, na kuua WaFalastina sita. Alisema mpaka wakati huo WaFalastina walikuwa hawajashambulia, wala kufyatua risasi dhidi ya Israel; lakini walilazimika kyfanya hayo, kwa mujibu wa Balozi wa Libya, kwa kujibisha uharamishaji wa Waisraili wa maafikiano ya kusimamisha mapigano.

Jean-Maurice Ripert, Mwakilishi wa Ufaransa katika UM alieleza kwamba wao wanaunga mkono azimio la Umoja wa Ulaya la wiki hii la kutafuta utaratibu wa kuhakikisha mapigano yanasimamishwa na kudumishwa. Vile vile azimio hilo limependekeza mashambulio ya makombora dhidi ya Israel yakomeshwe, bila masharti, na wakati huo huo kutaka operesheni za kijeshi za Israel zisitishwe katika eneo husika la WaFalastina; na kupendekeza hatua za dharura za kuhudumia misaada ya kiutu kwenye eneo la Ghaza ziendelezwe na jamii ya kimataifa.

Zalmay Khalilzad, Balozi wa Marekani katika UM aliarifu kuwa taifa lake linaunga mkono rai ya kusimamisha mapigano kwa haraka, pindi pendekezo hilo litaendelzwa na kuhishimiwa na makundi yote yanayohusika na mgogoro huo, akimaanisha Kundi la Hamas lazima likomeshe mashambulio yake ya makombora dhidi ya Israel. Alishikilia kwamba ilikuwa uamuzi wa Hamas kuchafua hali ya utulivukieneo, kwa kuanzisha mashambulio aliyoyaita ya makombora, ndio hali iliozusha vurugu na anaamini hali ina utata mzito, na kusisitiza haitoweza kusuluhishwa kwa kuandaa maazimio yalio sahili, yaliokosa wizani na yenye upendeleo wa upande mmoja.

Balozi wa Afrika Kusini, Dumisani Kumalo, yeye kwa upande wake, alisisitiza Baraza la Usalama linalazimika na kuwajibika kushtumu hadharani mashambulio ya vikosi vya Israel katika Ghaza na kulazimisha yasimamishwe haraka. Alisema Afrika Kusini imevunjwa moyo na uamuzi wa Serikali ya Israel wa kukataa mwito wa kimataifa wa kusitisha mapigano kwa saa 48 ili kuruhusu misaada ya kiutu na kihali kuingizwa Ghaza. Alisema Israel isitarajie kuwa itapata amani kwa raia wake na utulivu wa kisiasa wakati inaendelea kukalia kimabavu ardhi za WaFalastina, na kushikilia kulazimisha utawala huo kwa kutumia nguvu za kijeshi, dhidi ya umma wa WaFalastina wenye kupinga na kutokubali hali hiyo.

Wajumbe wenegine walioshiriki kwenye majadiliano haya ya Baraza la Usalama waliwakilisha mataifa ya Panama, Shirikisho la Urusi, Uingereza, Utaliana, Viet Nam, Uchina pamoja na Burkina Faso, Costa Rica, Ubelgiji na Kroashia. Vile vile mwakilishi wa Misri na Mjumbe Mwangalizi wa Umoja wa Nchi Huru za KiArabu walihutubia mkutano.

Wajumbe walioshiriki kwenye majadiliano yalioandama katika Baraza la Usalama walikubaliana kuhusu haja ya kusimamisha haraka mapigano, na kuyadumisha, halkadhalika, pamoja na kuhakikisha mahitaji ya kiutu yanahudumiwa, bila pingamizi, umma wa Ghaza. Wingi wa wajumbe waliozungumza katika Baraza la Usalama walitilia mkazo ya kuwa mzozo wa Ghaza hautofanikiwa kutatuliwa kwa kutumia mabavu ya kijeshi, na pia kusisitiza jumuia ya kimataifa inalazimika kutafuta suluhu ya kisiasa juu ya tatizo la Ghaza, kwa kuhamasisha makundi yanayohasimiana kushiriki kwenye majadiliano ya amani, kwa kupitia Baraza la Usalama.

Baraza la Usalama lilimaliza kikao bila ya kupiga kura.