Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Ijumanne magharibi, Baraza la Usalama limeitisha mkutano wa hadhara kuzingatia mgogoro wa Tarafa ya Ghaza. Kwenye taarifa yake mbele ya mkusanyiko huo KM Ban Ki-moon ametahadharisha kwamba mashambulio ya skuli za UM zinazotumiwa na mamia ya wakazi wa Ghaza kama maskani ya muda, yaliotukia Ijumanne ya leo na kusababisha vifo kadha vya raia, ni tukio linalomaanisha mapigano, na uhasama katika Ghaza, ni lazima yasimamishwe haraka iwezekanavyo kwa ajili ya utulivu na amani ya eneo. KM amesema anatarajia kuzuru Israel na maeneo yaliokaliwa ya WaFalastina wiki ijayo, na vile vile kuzuru miji mengine ya Mashariki ya Kati kutafuta suluhu ya kudumu ya amani ya eneo hilo.

Raisi wa WaFalastina, Mahmoud Abbas, ambaye alizungumza mbele ya Baraza la Usalama baada ya KM, aliyataka mataifa wanachama kukomesha haraka “maafa mapya” yaliowaangukia umma wa KiFalastina sasa hivi, chini ya mikono ya “mitambo ya maangamizi ya Israel”. Alisema “mauaji ya halaiki kwenye skuli za UNRWA katika kambi yawahamiaji ya Jabaliya ni ushahidi mpya wa uhalifu wa kuchukiza na kutisha” dhidi ya umma wa KiFalastina. Alitoa mwito wa kukomesha kile alichokiita “ushari wa Israel” ili kuweza kufufua tena majadiliano ya kisiasa ya kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati. Baraza la Usalama litaendelea na majadiliano yake kuhusu hali katika Tarafa ya Ghaza kesho asubuhi.

Watumishi wa UM saba walijeruhiwa hii leo pale jengo jirani na kituo cha afya cha UNRWA liliposhambuliwa na mabomu na kusababisha uharibifu mkubwa ambapo watu watatu kati ya hao walijeruhiwa vibaya sana pamoja na wagonjwa watatu wengine. Serikali ya Israel ilitahadharishwa katika siku za nyuma na UM kwamba operesheni za majeshi yao katika eneo la Tarafa ya Ghaza, zinahatarisha usalama wa majengo ya UM. KM ameripoti “kushtushwa sana” kwamba kuwa licha ya maonyo hayo, mara kadha wa kadha, msiba uliojiri leo hii haukufanikiwa kuzuilika, tukio ambalo KM alisema “lisiokubalika abadan” na kutaka “lisirudiwe” tena.

Josette Sheeran, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la UM juu ya Miradi ya Chakula Duniani (WFP) amelaani mauaji ya mfanyakazi wao, Ibrahim Hussein Duale, yaliotukia Ijumanne wakati alipokuwa akihudumia chakula umma muhitaji kwenye jimbo la Gedo, Usomali kusini. Kwa mujibu wa ripoti za WFP, majambazi watatu, walioficha nyuso zao na waliochukua bunduki, walimsogelea Duale wakati alipokuwa amekaa kitako, na kumlazimisha asimame. Bada ya hapo walimpiga risasi Duale na kumwua. Sheeran aliyakumbusha makundi yote kwamba wanawajibika kimataifa kuhakikisha wahudumia misaada ya kiutu waliopo kwenye eneo lao, huwa wanapatiwa hifadhi inayofaa dhidi ya mashambulio. Duale ni mtumishi wa tatu wa WFP kuuawa Usomali tangu mwezi Agosti 2008. Marehemu Duale amewacha mke na watoto watano. WFP inahudumia chakula watu milioni 1.5 katika Usomali.