Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hapa na Pale

Hapa na Pale

Msemaji wa KM leo ametoa taarifa maalumu iliosahihisha ajali iliotukia Alkhamisi, ambapo wafanyakazi watatu wa Shirika la UM la Kufarajia Wahamiaji wa KiFalastina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), walishambuliwa na vikosi vya Israel kwenye kituo cha mpakani cha Erez, karibu na Tarafa ya Ghaza. Watumishi hawo walikuwa wakiongoza msafara wa malori ya UNRWA yaliokuwa yamebeba misaada ya kiutu inayohitajika kukidhi mahitaji ya kimsingi kwa umma wa Ghaza. UNRWA inasema dereva mmoja wa msafara huo aliuawa; dereva mwengine alijeruhiwa vibaya kwenye tumbo, na dereva wa tatu alipigwa risasi mkononi. Kutokana na tukio hili UNRWA ilitangaza kulazimishwa kusimamisha shughuli zake, kukhofia usalama wa wafanyakazi. UNRWA ilisema haitoanzisha tena shughuli hizo mpaka pale wenye madaraka Israel watakapoahidi kihakika usalama wa wafanyakazi wa UM.

Kwenye mazungumzo ya kiwango cha juu, yaliofanyika Ijumaa Tel Aviv, kwenye Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Israel, maofisa wa UM waliarifiwa matukio yaliofanyisha UNRWA kusitisha baadhi ya shughuli zake Ghaza, hayaambatani na sera ya serikali, na Israel ilieleza kuwa ina masikitiko juu ya mashambulio hayo kutukia. Kwa hivyo, UM uliahidiwa kwamba usalama wa watumishi, majengo na operesheni zake za kuhudumia misaada ya kiutu zitaimarishwa vyema, na kutaratibiwa mawasiliano bora na vikosi vya Israel ili kuepukana na ajali dhdi ya watumishi wa UM waliopo Ghaza. UM umekumbusha makundi yote husika na uhasama majukumu yao, kwa kulingana na azimio la Baraza la Usalama 1860, ambapo yanatakikana kuruhusu, bila pingamizi, ugawaji wa misaada ya kunusuru maisha katika Tarafa ya Ghaza, na yanalazimika kusimamisha mapigano haraka, na kuhakikisha hali hiyo itadumishwa na kutekelezwa kama ilivyopendekezwa na azimio.

Tume ya wataalamu wa UM inatarajiwa kuzuru Nairobi na Addis Ababa wiki ijayo, ili kutathminia namna UM itakavyosaidia kuimarisha opersheni za vikosi vya ulinzi amani vya Umoja wa Afrika katika Usomali (AMISOM). Tume itajumlisha wajumbe kutoka Ofisi ya Masuala ya Kisiasa kwa Usomali, kutoka Idara ya Operesheni za Ulinzi Amani za UM, Idara za Kusaidia Nyanja za Mazingira ya Uhasama na kutoka Idara ya UM Inayohusu Masuala ya Kisiasa.

Siku ya tatu ya mazungumzo ya Nairobi baina Serikali ya JKK na kundi la waasi la CNDP yaliofanyika Ijumaa, yalilenga zaidi suala la usalama, ikijumuisha uwezekano wa kuandaa mapatano ya kusimamisha mapigano na kukomemsha uhasama, kwa mujibu wa taarifa ya Mpatanishi Mwenzi, Benjamin Mkapa aliyetoa baada ya kuakhirisha mazungumzo.

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) limeeleza, kwenye taarifa iliotangazwa Ijumaa, ya kuwa Bahari ya Mediteranian hivi sasa imegeuzwa kama “tariki ya kutafuta hifadhi ya kisiasa” kwa makumi elfu ya watu wanaokimbia mapigano na mateso kutokea Afrika. UNHCR inakadiria katika 2008 zaidi ya watu 67,000 walivuka Bahari ya Mediteranian kuelekea Ulaya; na nusu ya idadi hiyo waliwasili kwenye mataifa ya Utaliana na Malta, wingi wao kwa kupitia Libya. Asilimia kubwa ya wahamiaji hawa, ilisema UNHCR, waliomba wapatiwe hifadhi ya kisiasa, na nusu ya idadi hiyo walikutikana wanahitajia hifadhi jumla ya kimataifa.