Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majengo ya UM Ghaza yashambuliwa tena na kumkasirisha KM

Majengo ya UM Ghaza yashambuliwa tena na kumkasirisha KM

KM Ban Ki-moon leo anaendelea na ziara yake katika Mashariki ya Kati kutafuta uwiano kwenye juhudi za kuharakisha suluhu ya mapigano yaliopamba katika Tarafa ya Ghaza tangu tarehe 27 Disemba 2008.

“Kusema kweli, mambo kadha yalitukia. Jengo la UNRWA lililengwa na kupigwa moja kwa moja na mabomu, na kusababisha uharibifu usiosemeka, ambapo marisau ya mabomu yalijeruhi watu chungu nzima waliokimbilia kwenye majengo ya UM, kupata hifadhi dhidi ya mashambulio. Lakini tukio jengine la hatari liliojiri, kufungamana na shambulio hilo, lilihusika na mabomu ya kemikali ya fosfarasi yaliotupwa ndani ya majengo ya UM na kusababisha moto ambao bado unaendelea kuwaka – kama inavyofahamika ni shida kuuzima moto wa kemikali za fosfarasi. Kwa hivyo, tumelazimika kuhamisha malori ya nishati ya UNRWA yaliokuwepo hapo; tulibahatika kuyaondosha magari hayo katika mazingira yaliohatarisha sana maisha ya watumishi wetu, na tulikhofia moto usije ukaunguza zile ghala zetu ndogo zilipowekwa misaada ya chakula; lakini baadaye moto ulipamba kwenye zile ghala kuu za UNRWA, na kuunguza vitu vyote vilikuwemo ndani humo, hususan misaada ya chakula na zile ruzuku za kuhudumia misaada ya kihali, na kiutu, kwa umma muhitaji wa katika Tarafa ya Ghaza.”

Badaaye Waziri wa Ulinzi wa Israel, Ehud Barak, aliomba msamaha kwa KM kwa mashambulio ya vikosi vya Israel dhidi ya majengo ya UM katika Ghaza, tukio ambalo alisema lilikuwa ni “kosa la dhati” kwa upande wao, na alimwahidi KM kuwa hali hiyo haitorudiwa tena, na aliahidi pia kwamba hadhari kubwa zitachukuliwa katika siku zijazo kuhakikisha majengo ya UM na watumishi wake hawatoshambuliwa na vikosi vya Israel.

Kwa mujibu wa KM, kutokana na mazungumzo aliyokuwa nayo Misri wiki hii, alipata fununu kuwepo vipengele vyenye kubashiria vurugu katika Tarafa ya Ghaza litakomeshwa katika siku za karibuni. Alisema wakati umewadia kutekeleza haraka pendekezo la kusimamisha vurugu, na kuitaka jumuiya ya kimataifa kusaidia kurekibisha mazingira ya hali katika Ghaza, na kufuatilia tena yale mazungumzo ya amani yanayozingatia suluhu ya kuwa na Mataifa mawili kwenye eneo la mvutano, utaratibu pekee uliosalia wenye uwezo wa kuipatia Israel usalama wa kudumu. Alitilia mkazo kwamba mateso ya raia yamefikia kiwango kisichostahamilika kamwe, na kutaka makombora ya kienyeji dhidi ya Israel yakomeshwe, na vile vile kupendekeza mashambulio ya Israel katika Ghaza nayo yakome haraka, na wakati huo huo kuhakikisha umwagaji damu pamoja na mateso dhidi ya raia unasitishwa.

Kadhalika, kwa kutumia njia ya video, KM alipata fursa ya kuwasiliana leo na watumishi wa UNRWA waliopo kwenye majengo ya UM ya Tarafa ya Ghaza. Aliwashukuru kwa kazi yao ngumu, kwenye mazingira yalifunikwa na usumbufu na hatari kwa maisha yao. Alisema katika Alkhamisi aliwasiliana kwa simu kuhusu maendeleo kwenye juhudi za kidiplomasiya kuutatua mzozo wa vurugu katika Ghaza na Waziri wa Masuala ya Nchi za Kigeni wa Marekani Condoleezza Rice, Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown na Raisi wa Misri Hosni Mubarak, ambaye pia alikutana naye Cairo Ijumatano. Ijumaa KM anatazamiwa kukutana kwenye mji wa Ramallah na Raisi wa Falastina Mahmoud Abbas na Waziri Mkuu Salam Fayyad.